Home Simba SC YANGA : MNA CHIKWENDE, SISI TUNA FISTON ..TUKUTANE UWANJANI

YANGA : MNA CHIKWENDE, SISI TUNA FISTON ..TUKUTANE UWANJANI


YANGA wametamba kwamba kwa usajili waliofunga nao dirisha dogo hakuna wa kuwazuia kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara na Kombe la FA.

Hersi Said ambaye ni mmoja wa vigogo wa kamati ya usajili wa Yanga, amesisitiza kwamba usajili wa straika Mrundi, Fiston Abdulrazak ni funika bovu na wana uhakika kuwa kwenye mzunguko wa pili hawatazuwilika na Simba lazima wateme ubingwa na hawatakuwa na pumzi ya kumfunga Simba.

Hersi; “Tutamshughulikia kila atakayekuja mbele yetu, hakuna atakayebaki salama. Anakuja mchezaji atakayeongeza thamani kwenye safu ya ushambuliaji ya Yanga. Fiston anakuja kuweka sukari kwenye keki.” Lakini Kocha Cedrick Kaze amewasisitizia mashabiki kwamba huu ni muda wa kutembea kifua na kuvaa jezi ya Yanga bila kusita kwani yajayo ni makubwa na yanafurahisha.

Vigogo wa Yanga jana baada ya kujihakikishia usajili wa Fiston walikuwa wakiwatambia wenzao wa Simba wakiwakejeli kwamba ; “kama vipi tukatesti tena kwa Mkapa.”

Kocha mkuu wa Taifa Stars, Etienne Ndayiragije, alisema; “Ni wachezaji wazuri ambao kama watatumika vyema watazisaidia vilivyo timu zao kwani wameshathibitisha ubora huko walikotoka.”

“Mchezaji kama Fiston Abdulrazack aliyesajiliwa na Yanga, namfahamu vyema ni mchezaji mzuri na atawasaidia kutokana na uwezo wake na uzoefu alionao kwani amecheza katika ligi kubwa hapa Afrika,” alisema Ndayiragije.

Kocha wa timu ya taifa ya soka la ufukweni, Boniface Pawasa alisema; “Usajili wa dirisha dogo huwa ni wa wachezaji ambao wanaingia moja kwa moja kikosini sasa ukiangalia huu ambao ambao umefanywa na hizo timu, hao wachezaji wote wanaonekana wana nafasi ya kucheza na sio kukaa benchi.”

Usajili huu wa dirisha dogo kiufundi huenda ukaleta mabadiliko makubwa ndani ya Simba na Yanga.

YANGA

Kuanzia kwenye ulinzi, uimara na kuzoeana kwa mabeki Shomary Kibwana, Bakari Mwamnyeto, Lamine Moro na Yassin Mustapha huenda kukampa wakati mgumu beki mpya wa kati aliyenaswa kutoka Mtibwa Sugar, Dickson Job.

Uwezekano wa beki huyo kucheza unaweza kuja pale ambako mmojawapo kati ya Mwamnyeto au Moro anakosekana kikosini au iwapo benchi la ufundi la timu hiyo likaamua kutumia mfumo wa kuwa na mabeki watatu wa kati ambao unaweza kuwa ule wa 3-5-2 au 3-4-3./

Tofauti na Job, Ntibazonkiza na Abdulrazack wao usajili wao utakuwa na athari za moja kwa moja katika kikosi cha kwanza cha Yanga.

Uwezo wa Fiston katika kufumania nyavu, bila shaka utampa nafasi ya kuanza kama mshambuliaji wa kati katika mfumo wa 4-4-2 ambao Kocha Cedrick Kaze amekuwa akitumia na hivyo kupelekea Michael Sarpong kuwekwa benchi na nyuma yake atacheza Ntibazonkiza ambaye tayari ameshaitumikia timu hiyo katika mechi za Ligi Kuu na Kombe la Mapinduzi.

Sarpong anaweza asiumie peke yake kutokana na usajili huo kwani hata Deus Kaseke na Sogne Yacouba ambao  wamekuwa wakipata nafasi ya kuanza huenda wakajikuta wakilazimika kuwania nafasi moja ya kucheza ikiwa Fiston atatimiza kile kinachotegemewa.

Ntibazonkiza aliyeanza kuitumikia Yanga mwezi uliopita, tayari mchango wake ndani ya klabu hiyo umeshaanza kuonekana ambapo amehusika na mabao matano katika mechi tatu za Ligi Kuu walizocheza na timu za Dodoma Jiji, Ihefu na Prisons, akifunga mawili na kupiga pasi tatu zilizozaa mabao.

SOMA NA HII  RAMANI YA USAJILI YANGA YACHORWA NAMNA HII

Makali hayo ya Ntibazonkiza yakiongezewa nguvu na Fiston, yanaweza kuwa tiba la tatizo sugu la Yanga la ubutu katika safu yake ya ushambuliaji na inaweza kuanza kufunga idadi kubwa ya mabao ambayo itaiweka katika nafasi nzuri ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho la Azam msimu huu.

SIMBA

Sura mbili tatu mpya zilizoongezwa na Simba katika dirisha dogo la usajili, Lwanga Thadeo,Junior Lokosa na Perfect Chikwende zina nafasi ya kuingia moja kwa moja katika kikosi cha kwanza ikiwa wachezaji hao wataonyesha ubora ule ulioishawishi Simba iwasajili. 

Lokosa ni raia wa Nigeria ambaye inaelezwa kwamba kazi yake itakuwa ni kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa tu na amesaini mkataba wa miezi sita ambao akifanya vizuri kuna uwezekano wa kuongezewa. Mchezaji huyo alikuwa mfungaji bora wa Ligi ya Nigeria mwaka 2018. Simba watamtangaza muda wowote.

Uwepo wa Lwanga unamaanisha kwamba Jonas Mkude, Said Ndemla na Mzamiru Yassin wanatakiwa wafanye kazi ya ziada ili waendelee kupata nafasi ya kucheza.

Lwanga ameonyesha uwezo mkubwa wa kuilinda timu na kuichezesha na anaweza kufiti katika mifumo tofauti jambo linaloweza kulipa wigo mpana benchi la ufundi la Simba katika uteuzi wa kikosi chake kwenye mechi za mashindano mbalimbali.

Lakini Lwanga anaonekana atatibu udhaifu wa safu ya ulinzi ya Simba ambayo imeonekana kufanya makosa ya mara kwa mara pindi inapofikiwa kirahisi na washambuliaji au viungo wa timu pinzani na uwepo wake unaweza kuwa silaha ya kuufanya uwe salama mara kwa mara kutokana na jinsi anavyoweza kutibua mipango na kuziba mianya kwa wapinzani wasiweze kupenya kwenda langoni mwa timu pinzani.

Kwa upande mwingine, uwezo wa kufumania nyavu na kuchezesha timu wa Chikwende unategemewa na Simba kuwa chachu kwao kuwaongezea makali katika safu ya ushambuliaji ambayo imekuwa tishio kwa kupachika mabao katika Ligi Kuu msimu huu.

Chikwende anatazamwa kama mchezaji atakayesaidia kupunguza jukumu la upachikaji mabao kwa washambuliaji wa timu hiyo John Bocco, Chris Mugalu na Meddie Kagere kwani ana  uwezo wa kufumania nyavu hata akicheza katika nafasi ya winga au nyuma ya mshambuliaji.

Nyota huyo wa Zimbabwe, hadi amejiunga na Simba alikuwa ameifungia timu yake ya zamani ya FC Platinum jumla ya mabao mawili katika Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu.

Usajili wa Chikwende unamweka katika wakati mgumu Hassan Dilunga ikiwa Simba itaendelea kutumia mfumo wa 4-2-3-1 kwani anaweza kupangwa katika kundi la viungo watatu wanaocheza nyuma ya mshambuliaji lakini pia anaweza kutumika katika nafasi ya winga au mshambuliaji ikiwa watacheza mfumo tofauti na huo na hapo ushindani wa nafasi unaweza kuongezeka zaidi baina yake na Meddie Kagere ama Chris Mugalu.