CHAMA KUKOSA PENALTI KWA MKAPA, SIMBA WATOA TAMKO


 UONGOZI wa Simba umesema kuwa kukosa kwa penalti kwa nyota wao Clatous Chama pamoja na kushindwa kutumia nafasi walizopata jana mbele ya Azam FC ni sehemu ya mchezo ndani ya uwanja.

Ikiwa chini ya Kocha Mkuu, Didier Gomes, Uwanja wa Mkapa, Februari 7 ilitoshana nguvu kwa kufungana mabao 2-2 dhidi ya Azam FC huku nyota wao Chama akikosa penalti.

Penalti hiyo ilisababishwa na nyota wao Luis Miquissone iliokolewa na kipa wa Azam FC, Mathias Kigonya dakika ya 38.

Ofisa Habari wa Simba, Haji Manara amesema kuwa yote yanatokea ndani ya uwanja, jambo la muhimu ni kuangalia kwenye mechi zao zijazo.

"Mashabiki, wengi wanasema kuhusu sare na Azam FC, wanasahau kwamba tulikuwa tunacheza na timu bora, kukosa penalti ni sehemu ya mchezo hivyo mashabiki ningependa mtulie.

"Wengine wanasema kuhusu kukosa nafasi za wazi ambazo zimetokea ndani ya uwanja huwezi kulaumu kwa kuwa hata timu kubwa duniani huwa zinashindwa kupata matokeo ndani ya uwanja.

"Tunawapongeza wachezaji wetu wamefanya kazi kubwa ndani ya uwanja, hata wapinzani wetu pia wameweza kufanya kazi kubwa hivyo bado tuna kazi ya kufanya kwenye mechi zetu zijazo," amesema.

Simba imekusanya jumla ya pointi 39 ikiwa nafasi ya pili na imecheza jumla ya mechi 17 huku kinara akiwa ni Yanga mwenye pointi 44 amecheza mechi 18.Post a Comment

0 Comments