GOMES : HAO AL AHLY WAJE HATA KESHO


USHINDI wa bao 1-0 ilioupata Simba ugenini dhidi ya AS Vita ya DR Congo umempa mzuka Kocha Mkuu wa timu hiyo, Didier Gomes kwa ajili ya mchezo wao ujao wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Ahly ya Misri, akisema umemuongezea mzuka kwani haikuwa kazi rahisi.

Gomes alisema ushindi huo ni kwao utaongeza ari na morali kwa wachezaji katika suala la kufanya maandalizi ya kutosha kwa ajili ya mechi yao ya pili ya Kundi A dhidi ya Mafarao utakaochezwa Februari 23 jijini Dar es Salaam.

Kocha huyo raia wa Ufaransa alisema kuna makosa ambayo walifanya katika mechi hiyo na AS Vita ambayo wanakuja kuyafanyia kazi ili kuondokana nayo yasitokee tena katika mechi dhidi ya Al Ahly na Waarabu wengine watakaowafuata kwao Machi, Al Merreikh ya Sudan.

“Miongoni mwa makosa ni kupata nafasi za kufunga, tunakosa umakini wa kuzitumia, tunawapa mianya wapinzani ambayo kama wakiwa makini wanaweza kutufunga,” alisema.

“Hayo na mengine yote tutakwenda kuyafanyia kazi kwani katika mechi ya nyumbani dhidi ya Al Ahly itakuwa ngumu na yenyewe ushindani pengine zaidi ya hii kutokana na ukubwa pamoja na ubora wa hiyo timu ambayo ni yanne kwa ubora duniani. Kuna maeneo mengine ambayo tupo bora tunatakiwa kuboresha na kupaongezea hapo ili tuendelee kufanya vizuri kwa kila mpinzani ambaye tutakutana naye katika mashindano haya pamoja na yale ya ndani.”

Gomes alisema yeye na wasaidizi wake wametenga muda wa kutosha kuwaangalia Al Ahly ambavyo wanacheza na kuchunguza mambo mengi zaidi kutoka kwao na kwamba, atawapatia wachezaji wake ili kuona wanapata ushindi kujiweka katika nafasi nzuri ya kufuzu robo fainali kama walivyofanya msimu wa 2018-2019 wakati Simba chini ya Kocha Patrick Aussems aliyepo kwa sasa AFC Leopards ya Kenya.

“Unajua unapocheza na timu iliyokamilika kama Al Ahly sio kazi rahisi kuchukua pointi tatu iwe katika uwanja wao wa nyumbani au ugenini, tunatakiwa kufanya kazi ya kutosha kama benchi la ufundi pamoja na wachezaji ambao wanatakiwa kuwa na nia ya kufanya hivyo,” alisema Gomes.

“Tunarudi nyumbani Tanzania tukiwa katika hali nzuri kwani kile ambacho walituagiza kuja kukifanya huku tumekifanikisha.”

Post a Comment

1 Comments