INGIZO JIPYA YANGA LAOMBA KUJIWEKA KANDO


 FISTON Abdoul Razack ingizo jipya ndani ya kikosi cha Yanga inaelezwa kuwa aliomba akae pembeni kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Kagera Sugar, kutokana na presha za makelele za mashabiki wa Yanga.

Nyota huyo amecheza mchezo mmoja wa Ligi Kuu Bara, ilikuwa dhidi ya Mbeya City, kwenye sare ya kufungana bao 1-1.

Alicheza pia mchezo wa kirafiki dhidi ya African Sports wakati wakifungwa bao 1-0, Uwanja wa Azam Complex.

Habari kutoka kwa mtu wa karibu wa Yanga zimeeleza kuwa nyota huyo aliomba kutocheza mchezo huo ili aweze kurejea kwenye hali ya kawaida.

"Presha za mashabiki zimemfanya Fiston aombe kujiweka nje ya uwanja kwa muda ili arejee kwenye ubora wake.

"Jambo hilo lilimfanya akae pembeni kwani kwenye mechi mbili amekutana na joto ya jiwe la mashabiki ambao wamekuwa wakimlaumu kwa kushindwa kuipa timu hiyo matokeo," ilieleza taarifa hiyo.

Cedric Kaze, Kocha Mkuu wa Yanga amesema kuwa bado Fiston anahitaji muda wa kuweza kuzoeana na wachezaji pamoja na kuwa kwenye ubora wake.

"Ninatambua uwezo wa Fiston ambaye ni mchezaji mpya kadri siku ambavyo zinakwenda anazidi kuimarika hivyo nina amini kwamba atarejea kwenye ubora wake,".

Yanga ikiwa ipo nafasi ya kwanza kesho ina kazi ya kumenyana na Mtibwa Sugar kwenye mchezo wa ligi ambao ni mzunguko wa pili.

Mzunguko wa kwanza uliochezwa Uwanja wa Jamhuri, Yanga ilishinda bao 1-0 hivyo kesho utakuwa mchezo mkali kwa timu zote kusaka pointi tatu.Post a Comment

0 Comments