KOCHA AL AHLY: TUMEFUNGWA NA TIMU BORA


KOCHA mkuu wa kikosi cha Al Ahly raia wa Afrika Kusini, Pitso Mosimane amekiri kuwa katika mchezo uliopita dhidi ya Simba walipoteza mchezo kwa kufungwa na timu bora.

Simba juzi Jumanne katika dimba la Mkapa jijini Dar es Salaam ilifanikiwa kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Al Ahly, katika mchezo wa pili wa kundi A wa Ligi ya Mabingwa Afrika uliopigwa katika dimba la Mkapa jijini Dar es Salaam.

Kutokana na ushindi huo Simba imepanda mpaka kileleni mwa kundi hilo baada ya kuikusanyia pointi sita, na kuishusha Al Ahly mpaka katika nafasi ya tatu ya msimamo ikiwa na pointi tatu pekee.

Akizungumzia kipigo hicho, Mosimane amesema: “Kwanza kabisa nawapongeza Simba kwa ushindi walioupata, naweza kusema tulicheza dhidi ya timu bora tena ambayo ilicheza mpira mzuri kwenye kipindi cha kwanza.

“Ni wazi tulitarajia kuwa mchezo ungekuwa mgumu sana hasa kipindi cha kwanza, kutokana na kuwa na wakati mgumu wa kuzoea hali ya hewa.

“Kipindi cha pili hali ilikuwa nzuri zaidi kwani eneo kubwa la kiwanja kulikuwa na kivuli na hapo tulicheza vizuri zaidi na kutengeneza nafasi ambazo kwa bahati mbaya hatukuweza kuzitumia.

“Na ni wazi tunapaswa kujilaumu wenyewe kwani tulipaswa kutumia angalau nafasi moja tuliyoipata lakini mchezo huu umepita na sasa tunaangalia nafasi ya kufanya vizuri kwenye michezo ijayo,”

Post a Comment

0 Comments