KOCHA AZAM: TULISTAHILI KUIFUNGA SIMBA


KOCHA msaidizi wa klabu ya Azam, Vivier Bahati amesema kuwa anaamini kikosi chake kilistahili kuibuka na ushindi kwenye mchezo wao wa kiporo uliopigwa Jumapili iliyopita dhidi ya wapinzani wao Simba.

Katika mchezo huo ulioisha kwa matokeo ya sare ya mabao 2-2, Azam walionyesha kiwango kizuri hasa katika kipindi cha pili baada ya kuingia kwa Yahya Zayd na Mudathir Yahya ambapo walitengeneza nafasi nyingi lakini walishindwa kuzitumia.

Kwenye mchezo huo mabao ya Azam yalifungwa na Idd Selemani Nado na Ayoub Lyanga, huku Simba wao wakipata mabao yao kupitia kwa Meddie Kagere na Luis Miquissone. Sare hiyo inaifanya Azam sasa ifikishe michezo minne bila kupata ushindi mbele ya Simba. 

Bahati amesema kama washambuliaji wake wangekuwa makini kutumia nafasi walizotengeneza basi wangefanikiwa kuibuka na ushindi.

“Ulikuwa mchezo mzuri na wa ushindani, wapinzani wetu walikuwa na mchezo mzuri ndani ya kipindi cha kwanza wakitawala mchezo na kutengeneza nafasi, lakini tulivyokwenda mapumziko tuliongea na vijana wetu na kurekebisha makosa tuliyofanya.

“Na kila mmoja aliona jinsi tulivyocheza kipindi cha pili tuliweza kutawala na kutengeneza nafasi nyingi zaidi na kama washambuliaji wetu wangekuwa na utulivu wa kutumia nafasi tulizotengeneza basi nina uhakika tulikuwa tunastahili kuibuka na ushindi dhidi ya Simba,”

Sare hiyo imeifanya Azam sasa kufikisha pointi 33 zinazoendelea kuwaweka kwenye nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi baada ya kucheza mechi 18.

Post a Comment

0 Comments