YACOUBA : SIMBA SC NDIYO ILIYONIFANYA NIKATUA YANGA SC


UNAPOMTAJA Yacouba Songne, ni mmoja wa silaha kubwa katika safu ya ushambuliaji ya Yanga na katika mechi 17 zilizoiweka Wanajangwani hao kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Bara, raia huyo wa Burkina Fasso, amehusika.

Nyota huyo alipotua nchini na kujiunga na mabingwa hao wa kihistoria wa Ligi Kuu Bara hakuanza kasi, hivyo kudharaulika kabla ya baadaye kubadilika na kuonyesha uwezo mkubwa akifunga na kutengeneza nafasi za kufunga.

Gazeti Mwanaspoti lilimtafuta Songne na kufanya naye mahojiano na kufunguka mengi kuhusu maisha yake ndani ya Yanga.

MAJERAHA YAKE

“Kwa sasa kuna mabadiliko makubwa, ingawa bado sijawa sawa kwa asilimia mia moja. Hata hivyo, naendelea vizuri, ndio maana unaona nafanya mazoezi taratibu. Tofauti na tulivyotoka Zanzibar, maumivu yalikuwa makali zaidi, lakini naamini hali itakaa sawa,” alisema Yacouba akifafanua hali yake na mengine kuhusu maisha yake ikiwamo kuanza kwa kasi ndogo Yanga.

“Wakati nafika hapa sikuwa fiti sana, nilikuwa nimekaa nje kwa muda wa miezi minne bila kucheza kutokana na mlipuko wa virusi vya corona, pia utaelewa kwanza hapa nilikuwa nakuja katika timu mpya iliyokuwa na wachezaji karibu wote wapya, hivyo ilihitaji muda kuweza kukaa sawa ili niweze pia kuzoeana na wenzangu na hiki ndio kilitokea.

“Kama nilivyokwambia ilikuwa ni kuhitaji kuzoeana na wenzangu lakini binafsi nilijua natakiwa kuweka juhudi nilijituma na kuweka nguvu kubwa na maisha yakabadilika na kuanza kufanya vizuri ilikuwa rahisi kutokana na ushirikiano wa wenzangu kwa kuwa sote tulikuwa, tunahitaji matokeo mazuri.

PACHA NA KASEKE

Moja ya ushirikiano bora anaouonyesha Songne ni anapocheza na kiungo Deuse Kaseke na ushirikiano wao umekuwa ukizalisha mabao mengi sambamba na pasi za mwisho. Anaelezea siri hiyo.

“Mafanikio haya huwa yanaanzia mazoezini na huko tumekuwa tukielewana haraka na kila mmoja kumjua mwenzake, pia kocha naye amekuwa akituongezea kitu ili tuwe bora zaidi.

“Mimi ni mchezaji ambaye napenda kushirikiana na yoyote katika timu ninayoitumikia, sio lazima nifunge ingawa ni mshambuliaji. Nikiona mwenzangu anaweza kufanya hivyo, huwa nampasia, kikubwa timu ipate ushindi. Hivyo, ushirikiano wangu sio kwa Kaseke tu bali wachezaji wote.

DILI LA SIMBA

Alitua nchini baada ya kuingia kwenye rada za Simba na alicheza vyema kwenye mchezo wa ‘Simba Day’. Hata hivyo, baada ya mchezo huo aliibukia Yanga anayoitumikia mpaka sasa. Nini kilimkwamisha kucheza kwa wekundu hao?

“Ni kweli Simba ilikuwa ikinihitaji na tulionga zaidi ya mara moja. Hata hivyo, mpaka mwisho hatukufikia mwafaka, ndipo baadaye akaja meneja wangu na kunieleza Yanga wananihitaji,” anasema Yacouba na kuongeza;

“Niliridhika na ofa ya Yanga kwa sababu ilikuwa bora zaidi ya ile ya Simba na ofa nyingine na ndio maana niko hapa.”

Hata hivyo, alipoulizwa anadhani alifanya uamuzi sahihi kutua Yanga, naye anasema;

“Naweza kusema ndio, Yanga ni timu kubwa hapa Tanzania, ina rekodi nyingi nzuri za mafanikio. Angaalia sasa ndio tunaongoza ligi na tukiwa na timu bora, sioni kama naweza kuhisi sikufanya uamuzi sahihi. Nafurahia maisha ya hapa. Klabu hii pia ina mashabiki wanaopenda wachezaji wao na klabu yao. Wakati wote wanawahamasisha wachezaji kuhakikisha timu inashinda.”

Post a Comment

0 Comments