BOSI SIMBA: HATUACHI KITU KWA AS VITA


MAKAMU Mwenyekiti wa Bodi ya Simba Salim Abdallah ‘Try Again’ amesema wanajua pointi moja itawaingiza robo fainali ya Afrika lakini wanataka makubwa zaidi.

Abdallah alizungumza na gazeti la  Mwanaspoti Jijini Dar es Salaam na kusisitiza wanajipanga kumaliza shughuli kamili kwa kutaka kupata ushindi dhidi ya AS Vita Jumamosi ya Aprili 3, saa 10 jioni.

“Tumebakiza pointi moja tu ili tuingie hatua ya robo fainali ila Simba hii haitaki kuwa na malengo madogo kama hayo tumekubaliana tupate pointi tatu zote dhidi ya AS Vita,”alisema Abdallah ambaye ni mmoja wa waandamizi ndani ya uongozi wa Simba.

“Tukipata pointi tatu ina maana tutakuwa tumefikisha pointi 13 ambazo hakuna timu itakayoweza kuzifikia katika kundi letu lakini hapo tutahitaji kuwa kinara wa kundi ili tuwe na wakati mzuri katika upangwaji wa ratiba ya robo fainali.

“Malengo yetu haya sio tu yapo kwa mdomo lakini yatatanguliwa na vitendo zaidi kwa sasa tupo kwenye msiba wa Hayati Magufuli na tunajipanga ili tujue aina ya maandalizi yetu yatakuwaje.”

Alisema wanatambua sio kitu kigumu kwao kufika hatua ya robo fainali lakini wao kama bodi wanaangalia mbali zaidi ni jinsi gani wanaweza kupenya katika hatua ya robo fainali kwenda nusu fainali.

“Watu wasidhani kama hatua hii tumefika kwa kubahatisha tulijipanga vyema kufikia mafanikio haya na bado tunataka kufika mbali zaidi msimu huu huu kama Mungu atatupa baraka zake zaidi.

“Simba ina nafasi kubwa kuingia hatua ya robo fainali lakini hayo sio malengo yetu makubwa,tunataka kuvuka hapo ikiwezekana kufika nusu na kama ratiba itakuwa nzuri kwetu tuko tayari hata kucheza fainali.

“Tumewaambia wachezaji na tunawaamini kwamba wanatakiwa kujiandaa kwa hatua ngumu zaidi, tuliunda timu kama hii kwa kutafuta malengo makubwa kama haya ambayo tunayo sasa kama klabu,” alisema

Simba imekuwa na kiwango bora katika Ligi ya Mabingwa msimu huu wakishinda mechi tatu mpaka sasa katika hatua ya makundi na kutoa sare moja wakiongoza kundi lao A wakifikisha pointi 10 wakifuatiwa na Al Ahly wenye pointi 7, Vita wakiwa nafasi ya tatu wakiwa na pointi 4 huku Al Merrikh wakishika mkia wakiwa na pointi moja.

Post a Comment

0 Comments