Home Simba SC KAGERE :- TUFIKE ROBO FAINALI KWANZA ..MENGINE TUTAJUA BAADAYE

KAGERE :- TUFIKE ROBO FAINALI KWANZA ..MENGINE TUTAJUA BAADAYE


NA Meddie Kagere

KATIKA Ligi ya Mabingwa Afrika kama Simba tutafanya vizuri katika mechi zetu mbili za nyumbani, maana yake tutakuwa na uhakika wa kufuzu katika hatua inayofuata kama yalivyo malengo yetu.

Ukiangalia kwa hali ilivyo katika kundi letu unaweza kuona kuwa tayari tumeshafuzu hatua ya robo fainali, lakini tuna kazi kubwa ya kufanya.

Katika akili za wapenzi wengi wa soka nchini wanaamini hivyo kwa kuwa tuna mechi mbili katika uwanja wa nyumbani na aina ya matokeo ambayo tumekuwa tukiyapata nyumbani.

Mtazamo wangu unaamini tunaweza kufanya vizuri katika mechi za nyumbani kama ambavyo wengi wanadhani, lakini msimu huu timu nyingi zimepoteza matokeo kwao, hivyo yatupasa kupambana.

Ukiangalia hatujapoteza mechi yoyote ugenini licha ya kucheza mbili na ushindi nyumbani kama ilivyo kawaida.

Kwa hiyo tunatakiwa kutambua kama tuliweza kushinda na kupata sare ugenini hata wenzetu nao wanaweza kufanya hivyo katika uwanja wetu wa nyumbani.

Tunatakiwa kucheza kwa tahadhari kubwa katika mechi hizo mbili, lakini kufanya maandalizi ya kutosha kama timu na wachezaji binafsi ili atayepata nafasi aweze kuitumikia timu kwa nguvu.

Unajua halikuwa jambo rahisi kwa timu kama AS Vita kwenda kupata pointi ugenini – tena Misri dhidi ya Al Ahly – tusipofanya maandalizi ya kutosha na kucheza kwa umakini utakuwa mchezo mgumu kwetu.

Lakini tunatakiwa kulinda rekodi ya kufanya vizuri katika mechi za nyumbani sio kwa kuongea tu, bali kwenda kufanyia kazi pale uwanjani siku za mechi zetu za nyumbani.

Kwa namna ambavyo tumemaliza mechi zetu tatu za mzunguko wa kwanza kwa kuvuna pointi saba tuna nafasi kubwa ya kutafuta pointi nne ili tusonge katika hatua inayofuata.

Mechi hizi zinahitaji hesabu zaidi kwa ambavyo tutacheza nyumbani kwani itakuwa tofauti na zile mbili ambazo tumecheza ugenini.

Ukiangalia mechi zetu za ugenini muda mwingi tunacheza kwa kujilinda zaidi na kufanya mashambulizi ya kushtukiza katika lango la timu pinzani.

akini katika mechi zetu za hapa nyumbani hatutakuwa tunazuia zaidi, bali tutafanya mashambulizi mengi na kucheza kwa kujiamini. Tukumbuke msimu huu licha ya ugumu na timu mbalimbali kushinda katika viwanja vya ugenini, nasi moja ya silaha zetu ni kupata matokeo mazuri katika mechi za myumbani mbele ya mashabiki wetu.

SOMA NA HII  HIZI HAPA SABABU ZA NYUMA YA PAZIA KUHUSU PABLO KUSIMAMISHWA NA TFF...APIGWA FAINI YA MAMILIONI YA PESA...

Mara nyingi wachezaji wa Simba wanapoona wanacheza uwanja wa nyumbani – tena kuna mashabiki wengi kwa upande wetu wanakuwa juu zaidi na kuwa na morali ya kucheza kwa nguvu ili kushinda.

Ila mashabiki wanatakiwa kutokuwa na matokeo yao kutokana na tahadhari hiyo ambayo nimeeleza huko juu.

Licha ya ugumu, tahadhari niliyotoa na matokeo ya kushangaza kwa timu mbalimbali kubwa kushindwa kufanya vizuri, naamini tunaenda kucheza hatua ya robo fainali msimu.

Kiu yetu tumalize katika nafasi ya kwanza kwenye kundi ili kupata sio timu ya maana zaidi katika mechi za robo fainali ambazo tutacheza mara baada ya kumaliza hatua hii, bali timu shindani na bora inayopambana kwa ajili ya mafanikio.

Kama tukimaliza katika hatua ya kwanza, faida nyingine tutacheza mechi ya kwanza ya robo fainali ugenini na baada ya hapo tutakuja kumalizia mechi yetu ya pili nyumbani.

Kikubwa kwanza tufike katika hatua ya robo fainali na hapo ndipo tutaangalia malengo mengine baada ya kuwa na kitu mkononi mwetu.

Kwa namna ambavyo naiona timu yetu ilivyo msimu huu licha ya ugumu katika sehemu mbalimbali tunaomba mashabiki na Watanzania wote watuombee kwani tuna uwezo wa kufuzu katika hatua inayofuata.