KAZE :- SHIDA KUBWA YA YANGA NI UWEPO WA ''MABABA WAWILI'' WENYE KAULI SAWA


KOCHA aliyeachishwa kazi na Yanga wiki iliyopita, Cedric Kaze ameibuka hadharani kupitia gazeti la  Mwanaspoti na kueleza mambo mazito yaliyomkuta lakini akasema Kocha mpya ajaye (Hubert Velud raia wa Ufaransa) kama atapewa uhuru kiufundi atakuwa na kazi rahisi kwa vile ameshamrahishia uwanjani.

Kaze ambaye huenda akaondoka nchini leo kwenda kwao Burundi, aliiambia gazeti la  Mwanaspoti kwamba tatizo kubwa lililomfanya akayumba ndani ya Yanga ni kuingiliwa katika utendaji wake.

“Unajua lazima niseme wazi kabisa, familia moja haiwezi kuwa na baba wawili lazima itayumba, hakutakuwa na maelewano kwa vile kila mmoja atakuwa anatoa maelekezo yake na yatavuruga mambo.

“Ndani ya Yanga kuna baba wawili, wenye akili watanielewa. Kocha unakaa na wachezaji wako mnapanga hili anakuja baba mwingine huku anawaambia mengine, baba mwingine anapiga simu kwa wachezaji anazungumza vitu vya ajabu kabisa ambavyo vinavuruga umoja na kutengeneza makundi ya hapa na pale,” anasema Kaze

“Lakini uzuri ni kwamba wachezaji walikuwa wanakuja wananiambia kila kitu wanachoambiwa, mnakaa kikao cha mipango yako huku pembeni anakuja mtu mwingine naye ana mambo. Nilivumilia sana na nikawa nawaelewesha wachezaji wangu na uzuri walikuwa wananielewa, ingawa wakati mwingine binadamu unaelewa walivyo. Kwa hali hii ya muingiliano na watu kuingilia mambo ya kiufundi na wachezaji Yanga haiwezi kufika mbali.”

Kaze anasisitiza kwa kusema: “Ilifika mpaka wakati mtu anapiga simu eti usimchezeshe huyo ni Simba. Vitu vya ajabu kabisa kwenye hii dunia nimevikuta Yanga. Ninakaa nazungumza na wachezaji wangu, lakini mtu anapiga simu anachunguza kutaka kujua kitu hayo yanamhusu nini? Na akishajua anaanza kuingiza mambo yake mengine.

“Nataka niwaambie mashabiki na wanachama wa Yanga kwamba mimi Kaze niliipenda sana timu yao na nimefanya kila kinachowe zekana kuwapa raha ndio maana sijafungwa na Simba, nimewapa Kombe moja la Mapinduzi, nimeacha timu inaongoza ligi, wasiumie. Wasisononeke. Ila wasikitike jinsi timu yao inavyoendeshwa. Kocha yeyote hawezi kufanikiwa kama hapewi nafasi ya kuwa huru kwa mipango yake na wachezaji wake.

“Mimi ni kocha hata kama nisipoendelea kufanya kazi hii, nitafanya biashara zangu. Yanga itabaki milele, ubingwa wanaweza kuchukua msimu huu kwenye ligi hata FA, lakini waangalie muundo wa timu yao pande zote. Wanayanga wawe na maono ya mbali zaidi na nje ya timu yao, wajitahidi kuwa na watu sahihi na wanaojitambua kwenye nafasi walizowapa. Yanga ni kubwa sana lazima iwe na watu makini.”


Post a Comment

0 Comments