KOCHA AS VITA :- KWA SIMBA NI MIQUISSONE, LWANGA NA ONYANGO TU


KOCHA wa AS Vita, Raul Shungu bado haelewi kama kweli wamepokea kipigo cha mabao 3-0 dhidi ya Al Ahly ambayo waliibana vyema kwao na sasa wanatakiwa kuwafuata Simba. Lakini akasema ; “Huyo Luis hatari sana.”

Akizungumza kwa njia ya simu jana akiwa jijini Kinshasa, DR Congo Shungu alisema amekuwa kama amechanganyikiwa kwa kupoteza nyumbani dhidi ya Al Ahly.

Shungu alisema baada ya matokeo hayo wakati wakijiandaa kukutana na Simba ambao ndio vinara wa kundi lao alisema anawaza juu ya kuwakabili mastaa watatu wa wekundu hao Luis Miquissone, Thadeo Lwanga na beki Joash Onyango.

Kocha huyo wa zamani wa Yanga anayezungumza Kiswahili kizuri, alisema wachezaji hao watatu ndio silaha kubwa ambazo wekundu hao wameziongeza sasa ambazo zinawapa ubora wa kushinda mechi tatu.

Simba ndio vinara wa kundi A wakiwa na pointi 10 wakifuatiwa na Al Ahly wenye pointi 7, Vita (pointi 4) na Al Merreikh wakishika mkia wakiwa na pointi moja.

“Ukiangalia yule wa Msumbiji (Miquissone) ndio kila kitu kule mbele kwao, ana nguvu ya kupandisha mashambulizi na akili ya kufanya uamuzi wa haraka. Unahitaji akili na mpango mzuri kumzuia, tulijaribu kufanya hivyo hapa lakini mwisho tukafanya makosa ya kujisahau akaleta madhara,” alisema Shungu.

“Pale kati kuna yule kiungo mkabaji wa Uganda naye ameongeza ugumu katika kupita katikati anapambana sana na kuongeza uzito katika safu ya ulinzi yao na hata hapo nyuma kuna yule beki wa Kenya (Onyango) anacheza kwa akili sana.

“Ni lazima tuweze kujiandaa vyema kuweza kugeuza matokeo ila sio jambo rahisi lakini inawezekana, itategemea nao watafanya makosa gani,” alisema na kuongeza kama AS Vita watapasuka Dar es Salaam ndio biashara itakuwa imeisha.

Post a Comment

0 Comments