Home Simba SC MIQUISSONE :- SITAONDOKA SIMBA SC MPAKA…..!!!

MIQUISSONE :- SITAONDOKA SIMBA SC MPAKA…..!!!


STAA wa Simba, Luis Miquissone amewaambia mashabiki wa klabu hiyo kwamba kuna mambo makubwa kwake atayaonyesha uwanjani  kwani ndio kwanza anaanza.

Lakini akatoa msimamo wake kwamba haondoki Simba mpaka wao waridhie.

Luis ambaye anahusishwa na klabu mbalimbali za Arabuni, amefanya mahojiano maalumu na gazeti la Mwanaspoti nchini Sudan na kueleza mambo kadhaa ikiwemo hatima yake ndani ya Simba iliyomsajili kwa mkataba wa miaka mitatu na nusu akitokea UD Songo.

“Nipo na mkataba wa miaka miwili na Simba na si sahihi kufanya lolote na timu nyingine kuhusu suala la mkataba wangu kwani Simba wao ndio wenye mamlaka na jambo hili.

“Nimeona mawakala wengi kutoka Ulaya na Afrika tena katika timu kubwa wameonyesha nia ya kunitaka, kuna wengine mpaka wanampigia (simu) wakala wangu, kimsingi hilo si jambo sahihi,” anasema Luis.

Anasema hao mawakala kutoka Ulaya na Afrika wamekuwa wakimfuatilia kutokana na ubora ambao anauonyesha wakati huu, lakini watambue bado ana mkataba wa Simba.

“Wanatakiwa kwanza kuwafuata Simba na kuzungumza nao ili kama watakubali wawapatie thamani ambayo wanahisi ni sawa kutokana na mkataba uliobaki na hapo ndio nitakubali kukaa mezani,” anasema.

“Simba wao ndio wenye mamlaka juu ya kuniachia na kwenda katika timu nyingine kwani nipo na mkataba nao mpaka utakapomalizika, hapo naweza kuwa na maamuzi yangu binafsi, lakini wakati huu siwezi kueleza lolote.

“Nimeona timu kubwa za hapa Afrika kama nchi za Misri, Morocco, Afrika Kusini pamoja na zile za Ulaya lakini sina mamlaka na hili kwa kusema lolote mpaka hapo Simba watakaponiita mezani.

“Unajua haya yote yanazungumzwa kwa kuwa Simba inafanya vizuri na mimi nipo katika kiwango bora wakati huu, ila hawajui nimejipanga kufanya hivyo zaidi ya sasa.”

LIGI YA MABINGWA

Akizungumzia Ligi ya Mabingwa, Luis anasema: “Kama tukianza na nguvu hii katika mechi za mzunguko wa pili mbili tu ambazo tutacheza nyumbani, nina imani tutakuwa tumekamilisha zoezi la kufuzu.

“Bado tuna safari ndefu kwani katika mashindano haya kuna timu nyingi ambazo zimejipanga vya kutosha tunakwenda kushindana nazo, bado tuna mlima mrefu wa kupanda, lakini kikosi cha Simba na maandalizi yetu ambayo tunayafanya nina imani msimu huu timu itafika mbali katika mashindano haya.”

SOMA NA HII  KWA SOKA LA SIMBA YA MBRAZILI...IPO SIKU KUNA TIMU ITAKULA 20... HUYO NTIBAZONKIZA KAMA MPYAA...

MAISHA YAMEBADILIKA

Katika hatua nyingine staa huyo wa Simba, anasema maisha yake ambavyo yalikuwa hapo awali ni tofauti kabisa na wakati huu anaocheza Simba.

“Sio vyema kueleza hapa lakini maisha yangu yamebadilika kutokana na mafanikio ambayo nimeyapata ndani ya Tanzania hata nyumbani kwetu Msumbiji ambapo familia yangu ilipo,” anasema.

“Ndio maana unaona ninapokuwa uwanjani huwa naipigania Simba kwa nguvu zangu zote ili iweze kupata kile ambacho inahitaji kwani natambua mahala iliponitoa.

“Naamini kwa ushirikiano pamoja na wachezaji wenzangu kwa muda ambao nitakuwa Simba nipo katika timu sahihi ambayo tutapata mafanikio mengi kama tutaweza kuifikisha timu katika malengo yake.

“Naishi vizuri nikiwa nje ya kambi – kwa maana ya maisha yangu mwenyewe, lakini ndani ya kambi ndio sitamani hata ivunjwe, natamani kuwa na wachezaji wenzangu muda wote,” anasema.

“Tumekuwa tukiishi kwa kupendana, kupeana ushirikiano yaani kama familia moja jambo ambalo awali sikujua kama naweza kukutana nalo maana nilikuwa sifahamu kitu.

“Changamoto huwa zinatokea ambazo lazima tunazipatia suluhisho, kama kipindi cha nyuma nilikuwa sifahamu lugha ya Tanzania (Kiswahili), lakini sasa kwa kiasi fulani naelewa.

Kuhusu tofauti ya makocha Sven Vanderbroeck na Didier Gomes mchezaji huyo anasema kila mmoja yupo tofauti na mwenzake.

“Unajua kila kocha huwa na mbinu zake katika ufundishaji wake, kwa hiyo wakati wa Sven kuna mambo ya kiufundi ambayo nimeyachota kama ambavyo itakuwa kwa Didier Gomes ambaye tupo naye wakati huu.

“Wote ni makocha bora ndio maana Simba umewachukua ili kuhakikisha tu tunapambana wote kwa pamoja ili kufikia malengo ambayo timu imejiwekea kwa muda wote,” anasema Luis ambaye mashabiki wa Simba wanavutiwa na machachari yake.