MORRISON APEWA UJUMBE WA KUFANYIA KAZI NA MFARANSA WA SIMBA

 


KOCHA Mkuu wa Simba Didier Gomes amesema kuwa kiungo wake mshambuliaji Bernard Morrison ana uwezo mkubwa ila anapaswa aongeze umakini zaidi akiwa uwanjani.

Gomes, raia wa Ufaransa amesema kuwa amekuwa akifurahishwa na wachezaji wake wote wakiwa kwenye majukumu yao ila wakati mwingine Morrison amekuwa ni mtu mwenye utani mwingi.

Morrison alikuwa sehemu ya kikosi kilichowavaa Al Merrikh Uwanja wa Mkapa wakati wakishinda mabao 3-0 na kuwafanya wasepe na pointi tatu huku yeye akitengeneza pasi moja ya bao kwa Mohamed Hussein.

Kiungo huyo alikuwa kwenye ubora wake na alionekana kuwa na maamuzi ya haraka jambo lililomfurahisha Gomes.

Kuhusu uwezo wa mchezaji huyo Gomes amesema:"Morrison ni mchezaji mzuri ila kuna wakati mwingine amekuwa ni mtu wa utani, sasa ikiwa timu inahitaji ushindi ni lazima utani uwekwe kando kisha kazi ifanyike.

"Kila mchezaji ndani ya Simba ana uwezo wake na wanategemeana katika kusaka ushindi, bado safari ni ndefu kwani tunahitaji pointi moja ili kufikia malengo ya kutinga hatua ya robo fainali na haitakuwa kazi rahisi ikiwa kutakuwa na utani," amesema.

Aprili 3, Simba itakuwa na kibarua cha kusaka pointi tatu mbele ya AS Vita mchezo utakaochezwa Uwanja wa Mkapa.Post a Comment

0 Comments