Home Azam FC AZAM FC: HATUTATOKA MIKONO MITUPU MSIMU HUU

AZAM FC: HATUTATOKA MIKONO MITUPU MSIMU HUU


 UONGOZI wa Azam FC umeweka wazi kwamba msimu huu wa 2020/21 hawatatoka mikono mitupu watapambana kutwaa taji lolote lile katika mashindano makubwa ambayo wanashiriki.


Kikosi hicho kinachonolewa na Kocha Mkuu George Lwandamina, msimu uliopita wa 2019/20 kiliukamilisha bila taji kwenye kabati lao ambapo hata lile la Mapinduzi kilipokwa na Mtibwa Sugar iliyoinyoosha Simba bao 1-0 kwenye mchezo wa fainali.

Ofisa Habari wa Azam FC, Zakaria Thabit alisema kuwa msimu huu wapo kipekee na wamejipanga katika kila idara kuhakikisha kwamba wanapata taji.

“Msimu uliopita haukuwa mzuri kwetu, yale makosa tumeyafanyia kazi ila kwa msimu huu hamna namna lazima tuondoke na taji moja katika mashindano yote makubwa ambayo tunashiriki na ikiwezekana yote kwani uwezo tunao.

“Hapa nazungumzia taji la Kombe la Shirikisho pamoja na Ligi Kuu Bara, ukiangalia kwa namna ambavyo tunafanya kuna jambo letu ambalo tunahitaji kukamilisha, mashabiki watupe sapoti,” alisema Thabit.

Kwenye Kombe la Shirikisho Azam FC imetinga hatua ya  robo fainali baada ya kushinda mabao 2-1 dhidi ya Polisi Tanzania huku kwenye ligi ipo nafasi ya tatu ikiwa na pointi 54 baada ya kucheza mechi 28.

Mataji yote mawili kwa sasa yapo mikononi mwa Simba inayonolewa na Kocha Mkuu, Didier Gomes, raia wa Ufaransa.

SOMA NA HII  MATAJIRI AZAM FC WAPANGA KUITIBULIA SIMBA DILI LA KUMRUDISHA ADEL...WAMFUATA NA MKATABA MNONO...