Home Yanga SC KIGOGO YANGA- TUNAPASWA KUWAIGA SIMBA SC KIMATAIFA

KIGOGO YANGA- TUNAPASWA KUWAIGA SIMBA SC KIMATAIFA


YANGA imeangalia mwendo wa Simba kimataifa na matokeo dhidi ya Kaizer Chiefs kwa Mkapa wakagundua kitu na kutamka kuna mambo ya kuyachukua kutoka kwa watani zao hao ili kufika kimataifa.

Simba ilitolewa kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Kaizer kwa kufungwa jumla ya mabao 4-3, matokeo yaliyochekelewa na baadhi ya mashabiki wa Yanga kutokana na utani wao.

Wakati utani ukitawala juu ya matokeo hayo, kigogo mmoja wa zamani wa Yanga amesema yapo mambo ya kuchukua kutoka kwa Wekundu hao kwa kile walichokifanya Kimataifa msimu huu.

Aliyetoa mtazamo wake ni aliyekuwa bosi wa Kamati ya Mashindano wakati Yanga inafika kwa mara ya mwisho hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika, Hussein Nyika na kudai wanaicheka Simba kutolewa kiutani lakini kuna kitu wanaikumbusha Yanga yao.

Nyika ameliambia  gazeti la Mwanaspoti katika mahojiano maalum, Simba imelinda heshima yao kwa kuhakikisha msimu huu hawapotezi nyumbani licha ya kutupwa nje ya mashindano hayo na kama Yanga itapata tiketi ya kurejea Kimataifa msimu ujao basi ina kitu cha kujifunza.

“Nimeangalia mtani (Simba) hajapoteza nyumbani msimu huu, hii ni rekodi bora sana kwao inayowafanya kulinda hadhi yao. Nilichogundua, Simba ni wamoja, hawabaguani inapokuja suala la kulinda heshima ya klabu yao.

“Hapa lazima Yanga wenzangu tujifunze kupitia hili hata kama kafanya Simba, hata wao walijifunza kutoka kwetu katika kutulia na kusajili timu tishio wakiachana na kutumia wachezaji watoto.

“Yanga wenzangu baadhi tunatakiwa kuwa wa kweli pia tuwe na malengo katika yale tunayotaka tushinde na mipango yetu tuisimamie sawasawa na kama tutapata tiketi ya kurudi Kimataifa basi hapa ni sehemu ya kuanzia kwa kujitathimini wenyewe ndani na tuje mpaka nje,” alisema Nyika.

Alisema mashabiki wa Simba na viongozi wao walikuwa nyuma ya timu yao kwa kuishangilia na sio kuongeza presha kitu ambacho mwisho wa mchezo licha ya kutofuzu lakini walijikuta wanapongezana.

“Kuna wakati mashabiki wanaongeza presha mbaya kwa wachezaji na wanasahau ujio wao uwanjani ni kuja kuipa nguvu timu na sio kuwarudisha chini vijana wao, Simba walikuwa sambamba na wachezaji wao na kuwasaidia kupata mabao yale matatu.

SOMA NA HII  UBABE WA YANGA UPO KWENYE UTATU HUU WA MAP

“Waliwashangilia muda mrefu lakini kilichonivutia ni mwisho wa mchezo wote waliwapongeza wachezaji wao hali ile inamjenga mchezaji kujiona ana thamani ya kuzidi kuipigania timu yake.”

Nyika alieleza zaidi, hatua nzuri kwa klabu yao kujipanga vyema ni kuanzia mkutano mkuu ujao na uongozi wao unatakiwa kusikiliza wanachama wao kueleza wapi wamekosea lakini nao viongozi watoe tathimini yao.

Kigogo huyo ambaye pia aliwahi kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili alitaka pia umakini katika kusajili na alisema endapo watafanya makosa mengine yatawarudisha nyuma zaidi.

“Usajili ni kamari, sawa kuna maeneo unaweza kufanikiwa na usifanikiwe lakini tunatakiwa kuwa makini kama wenzetu walivyofanya miaka ya karibuni, kuna kazi bora imefanyika katika klabu lakini inahitaji mwendelezo na utulivu zaidi kupata wachezaji sahihi zaidi, halitakiwi hili la kusajili kuwa la watu wawili watatu pia wanatakiwa kuwa na fikra za kuangalia jinsi eneo hili lilivyotukwamisha msimu huu.”

Atupa kombora

Nyika hakusita kutupa kombora Simba akisema hata kama imezisumbua klabu kubwa Afrika kimataifa lakini wasidhani watakapokutana na Yanga watakutana na makosa kama ya wageni hao.

“Yanga inawajua Simba na Simba inajua kuna Yanga, Yanga haiwezi kucheza na Simba kizembe wasidhani kama itafanya makosa kama yale ambayo hizi timu ngeni imefanya kuna maandalizi ya kucheza na Simba na tukikutana nao hizo timu zote zilizoumia zije zioni Simba inavyoumizwa.”

Timu hizo zitakutana katika mechi ya mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Bara, Julai 3 baada ya awali kuahirishwa mechi hiyo kutokana na mabadiliko yaliyotolewa ghafla na wasimamizi wa soka nchini ambao ni Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).