Home Simba SC SIMBA SC ‘FULL GADO’ KUICHAKAZA KAIZER CHIEF KESHO

SIMBA SC ‘FULL GADO’ KUICHAKAZA KAIZER CHIEF KESHO

 


KOCHA wa Simba, Didier Gomes ameweka wazi kwamba aliamua  kuiwahisha timu Afrika Kusini ili kukabiliana na hali ya baridi kali iliyopo nchini humo kwa sasa.

Simba wataikabili Kaizer Chiefs kesho Jumamosi saa 1 usiku kwenye mechi ya awali ya robofainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika na marudiano wikiendi inayofuata.

Gomes amesema kuwa hali ya hewa Afrika Kusini ni ya baridi tofauti na Tanzania, hivyo anaamini kufikia siku ya mchezo wachezaji wake watakuwa wamezoea hali hiyo.

Simba wametoka Dar es Salaam ambapo nyuzi joto 29, upepo unavuma km 19 kwa saa na unyevu ni 59% wakati Johannesburg nyuzi joto ni 16, upepo unavuma km 4 kwa saa na unyevu ni 42%.

Kwa namna hali ya hewa ilivyokuwa nchini Afrika Kusini ni sawa na hali ya Njombe ilivyo.

“Mara nyingi hatua kama hii timu zote zinacheza kwa mbinu nyingi kabla ya mchezo hata unapoendelea huwa zinabadilika hilo tumejipanga nalo.

“Tutacheza kwa kuwaheshimu wapinzani, kujilinda zaidi na tutafanya mashambulizi ya kushtukiza naamini hili linaweza kutusaidia kama tulivyofanya DR Congo tulipocheza na AS Vita na kushinda,” alisema Gomes.

“Mpaka tumefika hatua hii kubwa hatutakiwi kuwadharau wapinzani wetu kwani ni timu bora na hawakufika hapa kwa bahati mbaya ila tunaandaa mbinu za kuwa bora zaidi yao ili kuwazidi na kupata kile tunachohitaji.”

“Tangu tumefika hapa kila kitu kinakwenda vizuri, wachezaji wangu wote wapo katika hali nzuri ila tunafanyia kazi yale ambayo tunahitaji ili kwenda kupigana dakika 90,” alisema kocha huyo

Kwa upande wa Mratibu wa timu , Abbas Ally alisema kuelekea mchezo huo kila kitu kinaenda sawa na wachezaji wote 26 wako salama na tayari kwa mchezo huo.

“Timu ipo salama, kila kitu kinaenda sawa, hakuna figisu ya aina yoyote ile ambayo tumekumbana nayo, hata wachezaji wetu wako fiti na salama kwa ajili ya mchezo huo ili tuweze kupata matokeo mazuri,”alisema Abbas

Abbas alisema kocha mkuu amepanga muda wa mazoezi ambapo wanafanya mara moja kwa siku kuanzia saa 12 jioni ili kwenda sawa na muda uliopangwa kuchezwa mechi hiyo.

SOMA NA HII  TRY AGAIN : MSIMU UJAO SIMBA SC TUTAKUWA NA KIKOSI BORA ZAIDI

“Hata mazoezi tunafanya saa 12 jioni sawa na saa 1 jioni kwa Tanzania, lengo ni kuendana na muda ambao mechi itachezwa, tuko vizuri tunahitaji matokeo mazuri tuna imani tutafanya vizuri japokuwa tunawaheshimu wapinzani wetu,”alisema.

Simba mara baada ya mechi hiyo, watacheza mechi ya marudiano kwenye Uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam Mei 22 na mshindi atakuwa ametinga hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo.