YANGA: TUNA ASILIMIA KUBWA YA KUSHINDA MBELE YA SIMBA


 MSHAMBULIAJI wa Yanga, Michael Sarpong, amesema kikosi chao kimejiandaa vizuri kuibuka na ushindi katika mchezo wa Kariakoo Dabi dhidi ya Simba Jumamosi hii kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar.

Wakati Sarpong akisema hayo, wenzake Farid Mussa na Abdallah Shaibu ‘Ninja’, nao wamedai kuwa Yanga ina asilimia kubwa ya kushinda.


Dabi hii ni mzunguko wa pili ambapo Simba itakuwa mwenyeji wa Yanga, raundi iliyopita watani hao walitoka sare ya 1-1, bao la Yanga likifungwa kipindi cha kwanza na Sarpong kwa mkwaju wa penalti baada ya beki wa Simba Joash Onyango kumchezea faulo Tuisila Kisinda na baadaye kusawazisha makosa yake kwa kufunga kwa kutumia kichwa.


Watani hawa wa jadi, wanatarajiwa kukutana huku Simba ikiongoza ligi kwa kuwa na pointi 61 na viporo viwili, wakati Yanga wanakamata nafasi ya pili kwa kuwa na pointi 57.


“Najua mchezo utakuwa na upinzani mkubwa sana ila tumejipanga kuweza kushinda na tuna uhakika tutashinda,” alisema Sarpong.


“Mechi itakuwa ngumu sana kama ilivyo kawaida zikikutana timu hizi mbili zenye ushindani mkubwa ila chochote kinaweza kutokea tusubiri tu matokeo,” alisema Farid.


“Tumejiandaa sisi kama wachezaji ili kuhakikisha tunapata ushindi, ni kweli raundi ya kwanza tulitoka sare, makosa tuliyoyafanya tutajirekebisha na hatutayarudia ili kuweza kupata ushindi, tumejipanga vizuri maana tunaona tunaweza kushinda,” alisema Ninja.Post a Comment

0 Comments