BOCCO 'APIGANA' KISA GADIEL MICHAEL..AWAELEZA VIONGOZI SIMBA SC A-Z


KIKOSI cha Simba kinaendelea na mazoezi kujiandaa na mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Polisi Tanzania, huku nyuma nahodha wa timu hiyo, John Bocco ‘Adebayor’ amedaiwa kutia mkono kwenye usajili wa klabu hiyo ili kutengeneza timu imara.

Nahodha huyo, aliyeifungia timu hiyo mabao 13 hadi sasa Ligi Kuu, inadaiwa ameushawishi uongozi kumbakisha beki wa kushoto, Gadiel Michael, mmoja wa wachezaji wanaomaliza mikataba yao Simba na waliokuwa kwenye hatihati ya kuendelea kubaki Msimbazi.

Bocco aliyecheza na Gadiel walipokuwa Azam FC, inadaiwa alipendekeza mabosi wa Msimbazi wambakishe beki huyo asiye na namba kikosi cha kwanza.

Mabosi hao fasta waliamua kuanzisha mazungumzo na Gadiel pamoja na wakala wake, ili asaini dili jipya kama wenzake waliomaliza mikataba yao.

“Bocco ndiye aliyekuwa akipushi ili Gadiel asalie Simba kutokana na anavyojituma mazoezini licha ya kukosa nafasi ya kucheza. Viongozi wamezingatia hilo na kwa sasa bado yeye tu kwenda kusaini,” kilisema chanzo.

“Kocha wetu awali alituambia anatamani kuona wachezaji wake wote wazawa wanabaki labda itokee kuna mmoja ametaka kuondoka mwenyewe,” alisema mtoa taarifa huyo aliyeomba kuhifadhiwa jina lake.

“Kimsingi baada ya mambo yote mazungumzo yameshafungwa na pande zote mbili zimekubaliana ila kinachosubiriwa hapa Gadiel kupewa taarifa ya kwenda kusaini mkataba na jukumu litabaki kwake kama ataongeza au atakuwa na jambo lingine.”

Hata hivyo, taarifa nyingine za watu wa karibu wa mchezaji huyo zinasema Gadiel pamoja na kukubaliana na mabosi hao kwenye mazungumzo, lakini akili yake bado inafikiria kuondoka kwa sababu ya kukosa nafasi ya kucheza tangu aliposajiliwa akitokea Yanga msimu miwili iliyopita.

Kama Gadiel ataamua kusaini Simba itamfanya awe mchezaji wa saba wa kizawa waliongezwa mkataba baada ya Kennedy Juma, Mohammed Hussein, John Bocco, Shomary Kapombe, Benno Kakolanya na Erasto Nyoni, wakati kwa upande wa wageni ni Meddie Kagere na Pascal Wawa, huku Joash Onyango naye mambo yakielezwa yapo freshi.

Simba pia inaelezwa wapo kwenye mawindo ya kuwanasa kiungo mmoja kutoka Mali na straika mmoja kati ya Justin Shonga na Moses Phiri wanaokipiga Afrika Kusini na Zambia katika njia ya kuimarisha kikosi chao kilichofikia robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu.

SHIVA NA AJIBU

Wakati dili la Gadiel likiwa hivyo, wachezaji wengine watatu wazawa ambao mikataba yao nayo ipo ukingoni, wapo kizani.

Wachezaji hao ni Miraj Athuman ‘Sheva’, Ibrahim Ajibu na kipa Ally Salim mambo yao, ingawa inaelezwa hata wao wanaweza kubakishwa kutegemea na maamuzi ya mabosi wa juu kulingana na mahitaji ya kocha wao, aliyerejea juzi usiku tayari kuwapa nyota wake mbinu mpya kumalizia msimu.

Gomes alikuwa mapumzikoni Ufaransa baada ya kumalizika kwa mchezo wao wa kiporo cha Ligi Kuu Bara dhidi ya Ruvu Shooting na jana alitarajiwa kuanza kuwapigisha tizi wachezaji wake ambao kwa wiki nzima walikuwa chini ya Aden Zrane na Milton Nienov.

Post a Comment

1 Comments