HII HAPA RODHA YA NYOTA WALIOMALIZANA NA YANGA MAZIMA


INASEMEKANA Yanga imemalizana na nyota 
wawili kwa siri kubwa katika kuelekea usajili wa msimu ujao ambao wamepanga kubeba makombe yote watakayoshindania.

Wachezaji hao ni kipa wa Tanzania Prisons, Jeremia Kisubi na Dickson Ambundo anayekipiga Dodoma Jiji.

Yanga hadi hivi sasa wachezaji waliofanikiwa kuwasajili na kuwapa mikataba ya miaka miwili kwa siri ni David Bryson anayeichezea KMC FC na beki wa AS Vita, Shaaban Djuma.

Kwa mujibu wa chanzo cha habari kutoka ndani ya uongozi wa Yanga, imefikia makubaliano mazuri na Kisubi na Ambundo ambao tayari wamepewa mikataba ya awali ya kuichezea timu hiyo.

Chanzo hicho kilisema kuwa wachezaji hao wanachosubiria ni kumalizika kwa ligi mikataba yao ikiwa imemalizika tayari kwa ajili ya kujiunga na Yanga.

Kiliongeza kuwa timu hiyo inataka kumsajili Kisubi kwa ajili ya kuiimarisha safu yao ya magolikipa wao baada ya tetesi kuzagaa Yanga kuwepo katika mipango ya kuachana na Mkenya, Farouk Shikalo.

“Katika msimu huu Yanga imepanga kufanya usajili mkubwa wa wachezaji wapya baada ya kujihakikishia nafasi ya kucheza michuano ya kimataifa, mwakani.

“Hivyo katika kukiboresha kikosi hicho, viongozi tayari wameanza usajili wa siri kwa kufanikisha usajili wa baadhi ya wachezaji kwa hofu ya usajili wao kuingiliwa.

“Kwani tayari imemalizana na wachezaji wawili mabeki wa pembeni Djuma wa AS Vita na Bryson anayeichezea KMC, pia uongozi upo katika hatua za mwishoni za kumsajili Kisubi na Ambundo ambao wanasubiria ligi kumalizika,” alisema mtoa taarifa.

Akizungumzia hilo, Mkuu wa Kitengo cha Habari cha Yanga, Hassani Bumbuli, alisema: “Suala lote la usajili hivi sasa lipo kwa kocha wetu Nabi ambaye yeye ndiye atakayesimamia zoezi zima la usajili na uongozi kazi yetu ni kufanikisha usajili.”Post a Comment

0 Comments