KISA SIMBA, DJUMA AKWAMA KUJA BONGO NA MAYELE


HABARI ikufikie kuwa uongozi wa Yanga
 
umeamua kubadili rasmi mipango ya kutua nchini kwa wachezaji Shabani Djuma na Fiston Mayele ambao walitakiwa kutua mapema wiki hii.

Yanga tayari ilikwishamalizana na Shabani Djuma ambaye alikuwa ni beki wa kulia wa AS Vita mara baada ya kumsajili kwa mkataba wa miaka miwili huku Fiston Mayele yeye akikiri wazi kuja kukamilisha dili na Yanga pindi atakapotua nchini sambamba na Shabani Djuma.

Chanzo chetu cha uhakika kutoka Yanga kimeliambia Championi Ijumaa kuwa sababu kubwa ya kubadili siku ya wachezaji hao kutua nchini ni uwepo wa fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam Sports (ASFC) dhidi ya Simba ambapo inaweza kuleta presha kwa wachezaji ambao wapo kwa sasa, hivyo ujio wao utakuwa mara baada ya kumalizika kwa fainali hiyo.

“Ilikuwa ni mipango yetu kuona wachezaji hao wanakuja na kushuhudia mchezo wa fainali dhidi ya Simba lakini tumeona itawaongezea presha kubwa wachezaji ambao wapo kwani kama ambavyo unafahamu kwa sasa ni mwisho wa msimu, kuna mambo ya kuachana na wachezaji na kuingiza wachezaji wapya.

“Hivyo baada ya kumalizika kwa mchezo huu, tunatarajia wachezaji hao kuingia hapa nchini kwa ajili ya taratibu mbalimbali za timu ikiwemo mipango ya maandalizi ya msimu ujao,” kilisema chanzo hicho.

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili wa Yanga, Dominick Albinus, alisema kuwa uongozi wa klabu hiyo hautarajii kumpokea mchezaji mpya yeyote ndani ya klabu hiyo kwa sasa labda mpaka kumalizika kwa mchezo wa fainali dhidi ya Simba mara baada ya ligi kumalizika.

“Ligi tayari ilishamalizika, kilichobaki kwa sasa ni kumalizika kwa mchezo wa Kombe la Shirikisho tutakaocheza dhidi ya Simba huko Kigoma, ndio mambo mengine yaweze kufanyika kwa kufuata taratibu maalumu zilizoandaliwa na uongozi wa Yanga.

“Kuhusu wachezaji wapya kuja kuutazama mchezo wa fainali dhidi ya Simba niseme hapana hakuna mpango kama huo kwa timu labda mpaka fainali hii itakapomalizika ndio tunatarajia kuona wachezaji wapya wakianza kutua nchini,” alisema kiongozi huyo.Post a Comment

0 Comments