MAKUSU ATAJWA KUINGIA ANGA ZA SIMBA

IMEELEZWA kuwa, Jean Marc Makusu Mundele yupo kwenye rada za mabingwa mara nne mfululizo ndani ya Ligi Kuu Bara ambao ni Simba.

Nyota huyo ambaye ni mshambuliaji ni mali ya AS Vita ya Congo na alikuwa akikipiga ndani ya Klabu ya Orlando Pirates ya Afrika Kusini kwa mkopo.

Nafasi yake ni mshambuliaji aliweza kufanya vizuri katika michuano ya kimataifa ambapo aliweza kutupia jumla ya mabao 19 katika michezo ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho ndani ya timu hiyo.

Habari zimeeleza kuwa nyota huyo yupo Bongo ambapo alitua kimyakimya ili kufanya mazungumzo na Simba inayonolewa na Kocha Mkuu, Didier Gomes. 

"Makusu amekuja nchini kwa ajili ya kuzungumza na viongozi wa Simba kabla ya kuja Dar alikuwa amesharudi kwao Congo akitokea Afrika Kusini ambapo alikuwa ndani ya Orlando Pirates inayoshiriki ligi huko Sauzi," ilieleza taarifa hiyo.

Kocha Msaidizi wa AS Vita ya Congo, Roul Shungu amesema kuwa hana taarifa juu ya mshambuliaji huyo kuja Tanzania ila anajua kwamba Simba inamuhitaji mchezaji huyo.

Mwenyekiti wa Simba, Murtaza Mangungu amesema kuwa masuala ya usajili bado wakati wake kwa sasa wamewekeza nguvu kwenye mechi zao ambazo zimebaki.


Chanzo: ChampioniPost a Comment

0 Comments