SIMBA KUTWA MARA MBILI, WACHEZA MECHI ZA KIRAFIKI


 UONGOZI wa Simba umeweka wazi kwamba kila siku wachezaji wao wanafanya mazoezi mara mbili kwa ajili ya maandalizi ya msimu mpya 2021/22 ili waweze kutetea mataji yao.

Kwa sasa kikosi cha Simba kimeweka kambi Arusha kikiwa chini ya Kocha Mkuu, Didier Gomes akishirikiana na Hitimana Thiery.

Akizungumza Kaimu Ofisa Habari wa Simba, Ezekiel Kamwaga amesema kuwa kambi inaendelea salama na wachezaji wanaendelea kupambana ili kuweza kuwapa furaha mashabiki wa Simba.

“Kwa upande wa kambi kila kitu kinaendelea vizuri na wachezaji wanaendelea na mazoezi ambapo kila siku wanafanya mazoezi mara mbili, asubuhi na jioni na muda mwingine itategemea mwalimu anahitaji kitu gani.

“Jambo la msingi ambalo tunahitaji kufanya ni kuona kwamba kuelekea Simba Day mambo yanakuwa na utofauti mkubwa. Mashabiki nao wameonyesha muitikio mkubwa kwa ajili ya tamasha  lao hivyo ni suala la kusubiri na kuona wale ambao hawajapata tiketi basi wafanye jitihada kuzipata,” amesema Kamwaga.

Simba kwa sasa inaendelea na kambi Arusha na imekuwa ikicheza michezo ya kirafiki ya ndani ilicheza na Coastal Union, Aigle Noir pamoja na Fountain Gate.Post a Comment

0 Comments