Ticker

6/recent/ticker-posts

DSTV BANNER

KUELEKEA MECHI YA SIMBA vs YANGA...UTAMU UKO HAPA...KOCHA YANGA AONYA KUHUSU MORRISON...


HOMA ya pambano la watani wa jadi huko mtaani imeanza kupanda huku mjadala mkubwa ukiwa ni mastraika dhidi ya mabeki wa timu hizo. Kila mmoja anatamba. Kwenye kikosi cha Simba wenyeji wa mechi hiyo wanamtazama, Bernard Morrison kama nyota atakeyekwenda kuwapa furaha kutokana na ubora wake wa hivi karibuni kwenye Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho Afrika.

Yanga mbali ya ubora wa wachezaji wao kwenye maeneo mengine kama Feisal Salum, Yannick Bangala, Khalid Aucho, Djigui Diarra wanaotazamwa kutoa burudani lakini wana nyota wao Fiston Mayele ambaye ni mtaalamu wa kutikisa nyavu.

UTAMU UPO HAPA

Simba tangu amekuja kocha, Pablo Franco amembadilishia majukumu Morrison na kumchezesha eneo la viungo watatu washambuliaji muda wote akiwa mchezaji huru asiyehusika zaidi kwenye kukaba kama ilivyo kuanzisha mashambulizi.

Morrison kutokana na kucheza huru nyuma ya mshambuliaji, Meddie Kagere maana yake atakuwa na kazi ngumu kupambana dhidi ya mabeki wanne wa Yanga, Djuma Shabani, Kibwana Shomary, Dickson Job na Bakari Mwamnyeto.

Kibwana atakuwa na jukumu la kwanza kumzuia Morrison mwenye uwezo wa kutengeneza nafasi za kufunga mabao kwa wachezaji wengine kama alivyofanya mechi mbili mfululizo dhidi ya Ruvu Shooting na Red Arrows ya Zambia.

Morrison sifa zake nyingine anaweza kufunga mabao aina mbalimbali kwa kichwa, miguu yote miwili pamoja na ufundi wa kupiga mipira iliyokufa faulo pamoja na kona zinazokwenda kuzaa mabao. Kama haitoshi staa huyo wa Simba kwa sasa ni mzuri kuwasumbua mabeki wa timu pinzani kutokana na uwezo wake wa kumiliki mpira na si rahisi kupokonywa jambo ambalo linamfanya kuchezewa rafu za lazima.

Kutokana na sifa hizo, Morrison anayetegemewa kuibeba Simba siku ya mechi ni Kibwana, Djuma, Mwamnyeto na Job muda wote watakuwa na kazi ya kuhakikisha hafungi bao, hafanyi hatari yoyote pamoja kumzuia kuonyesha makali.

Djuma, Kibwana, Job na Mwamnyeto kama wataweza kumzuia Morrison na kushindwa kuonyesha makali yake muda mwingi Simba wakienda kufanya mashambulizi maana yake watakuwa na uhakika wa kuondoka na ushindi katika mechi hiyo kama wakishindwa kufanya hivyo lolote linaweza kutokea langoni kwao kutokana na ubora wa Mghana huyo.

Tangu Morrison amesajiliwa kutokea Yanga akiwa ndani ya kikosi cha Simba hajawahi kuonyesha makali kwenye mechi ya Dabi na huenda wakati huu akatamani kufanya hivyo kutokana na kiwango bora alichokuwa nacho na majukumu makubwa aliyopewa katika timu ni wazi mabeki hao wa Yanga watakuwa na kazi dhidi yake. Lakini Morrison ambaye amewashinda Yanga kwenye kesi ya CAS hivikaribuni amesisitiza kwamba sasa miguu yake itaongea zaidi uwanjani na atawaonyesha ubora wake.

HUKU MAYELE KULE INONGA

Wakati Simba wakiamini Morrison atawabeba, Yanga jina ni moja tu, Mayele ambaye katika mechi saba walizocheza kwenye Ligi ameweka kambani mabao matatu. Fiston ana uwezo wa kufunga mabao kutokana na uchezaji wake ameweka kambani kwa vichwa, miguu kama alivyowafunga Simba bao moja katika mchezo wa Ngao ya hisani.

Kutokana na ubora huo wa Mayele kwenye kufunga mabao, ni wazi vitasa watatu wa Simba, Hennock Inonga anayerejea kikosi baada ya kumaliza adhabu, Pascal Wawa na Joash Onyango watakuwa na kazi ya kumzuia.

Inonga, Wawa na Onyango wawili kati ya hao ndio wataanza na jukumu la kuhakikisha Mayele hafungi wala kuonyesha makali yake yoyote litakuwa la kwao na wakifanikiwa maana yake Simba watakuwa salama ila wakishindwa atawaadhibu kama ilivyokuwa kwenye mechi ya Ngao ya hisani.

Mayele baada ya mechi na Mbeya Kwanza alisisitiza kwamba ana sapraizi kwa mashabiki wa Yanga kwenye mechi dhidi ya Simba na kila mchezaji amepania kuhakikisha wanaondoka na ushindi mzuri kwenye mchezo huo aliokiri kwamba utakuwa mgumu.

WASIKIE MAKOCHA

Kocha wa zamani wa Yanga, Luc Eymael alisema; “Mabeki wa Yanga ambao watakuwa na kazi ya kumzuia Morrison wanatakiwa kufanya maandalizi ya kutosha na umakini mkubwa uwanjani kwani ni aina ya mchezaji mwenye ubunifu mwingi wanakwenda kukutana nae.” 

Kocha wa zamani wa Yanga, Kenny Mwaisabula alisema kuwa; “Mabeki wa Simba wamekuwa na shida ya kushindwa kukaba mipira ya krosi na kumzui mshambuliaji mpaka mwisho na hivyo ndivyo Mayele anacheza kwahiyo wanatakiwa kubadilika kwenye mapungufu hayo,” Meddie Kagere amesisitiza kwamba mechi hiyo ni kama fainali yao.

Reactions

Post a Comment

0 Comments