Ticker

6/recent/ticker-posts

KISA KUFUNGWA NA AZAM..NABI ATUA TZ KWA 'HASIRA'..ATOA MAAMUZI MAZITO..SENZO AINGILIA KATI...


KAMA kuna watu walikuwa na stresi jana ni mastaa wa Yanga. Kocha Nesreddine Nabi amewapigia simu viongozi akawaambia; “Niwakute wachezaji wote kambini.”

Yanga walirejea Jijini Dar es Salaam juzi baada ya kutema Kombe la Mapinduzi mbele ya Azam, na akili yao ni kwamba wangekula bata juzi na jana uraiani. Lakini ghafla Nabi akafuta hilo akaamuru jana mchana (badala ya leo) wote wawepo kambini bila kuchelewa na jioni waanze kupasha.

Nabi ambaye alitua jijini Dar usiku wa kuamkia juzi,  ambapo akiwa Ubelgiji aliamuru viongozi wawarudishe wachezaji kambini haraka kwani kilichotokea kwenye mechi za Mapinduzi hakikumfurahisha na hakitoi nafasi ya kupumzika.

Kwa mujibu wa viongozi, Nabi amewaambia kwamba kutokana na anguko la kikosi chake kwenye Kombe la Mapinduzi hakuna haja ya mapumziko marefu kwani kuna mechi mbili ngumu ugenini dhidi ya Coastal Union na Polisi Tanzania ambazo msimu uliopita ziliwapotezea ramani ya ubingwa.

Hivyo jana mchana mastaa wote japo wakisonya chinichini wakalazimika kurejea kambini Avic kule Kigamboni kuendelea na matizi na yeye ataungana nao kwenye chai asubuhi hii.

Mabadiliko hayo ya Nabi yakaenda mbali zaidi akiwaambia mabosi wake kwamba kila mchezaji ambaye alipewa ruhusa muda umekwisha na hata kama yuko nje ya nchi anataka kumkuta kambini isipokuwa kipa wao Diarra Djigui pekee ambaye yupo nchini Cameroon katika Fainali za Mataifa Afrika na taifa lake la Mali.

Kaimu Mtendaji Mkuu wa Yanga, Senzo Mazingisa amethibitishia  juu ya mabadiliko hayo akisema pia hata wao viongozi hakuna anayekaa kwenye kiti akatulia na sasa kila mmoja akili yao ni kuelekea mchezo dhidi ya Coastal Union.

Yanga itakuwa na dakika 90 ngumu ugenini za kubadilisha upepo wakikumbuka hawajafanikiwa kushinda katika Uwanja wa Mkwakwani kwa muda mrefu sasa na hata msimu uliopita walianguka kwa mabao 2-1 na kuvurugiwa rekodi yao ya kutopoteza mechi 32 mfululizo za Ligi Kuu, ukijumuisha na za msimu uliotangulia. Walikuwa wakiifukuzia rekodi ya muda wote ya kutopoteza mechi 38 za Ligi Kuu inayoshikiliwa na Azam FC.

“Kocha ametaka kila mchezaji kuingia kambini, hakutakuwa na muda mrefu zaidi na wakiingia kambini ni moja kwa moja mpaka tutakapoondoka kwenda Tanga, tumekubaliana na ratiba hiyo,” alisema Senzo ambaye ni bosi wa zamani wa Simba.

“Hata sisi viongozi nasi tupo katika vikao vingi hakuna anayekaa chini akatulia akili zote zipo katika mechi hizo mbili, tunafahamu zitakuwa mechi ngumu katika afya ya malengo yetu ya msimu,” aliongeza raia huyo wa Sauzi.

Senzo alisema tayari kuna baadhi ya viongozi walishatangulia Tanga mapema kuhakikisha kila kitu kinakwenda sawa katika hesabu zao za mchezo huo kisha ule wa Kilimanjaro wakiwafuata Polisi Tanzania.

Hasira za Yanga zinatokana na kupoteza Kombe la Mapinduzi ambalo lilikuwa kwenye malengo yao ya msimu. Sasa wamebakiwa na makombe mawili lile la Shirikisho la Azam na Ligi Kuu Bara ambako ushindani ni mkubwa.

Coastal wako vizuri zaidi msimu huu wakishikilia nafasi ya nne sasa katika msimamo na waliwavimbia Simba kwa sare ya 0-0 kwenye Uwanja wa Taifa katika mechi yao ya Okt.31, 2021.

Reactions

Post a Comment

0 Comments