Ticker

6/recent/ticker-posts

VITA YA SIMBA NA AZAM YAHAMIA AFCON LEO...NI PETER BANDA vs PRINCE DUBE..


Mchezo baina ya Zimbabwe na Malawi kwenye fainali za Afcon leo unaweza kutafsiriwa kama debi ya Simba na Azam kwenye fainali hizo za Taifa kutokana na timu hizo mbili kuwa na nyota wanaocheza katika klabu hizo za soka nchini.

Kwa upande wa Zimbabwe, nyota watatu wa Azam FC, Bruce Kangwa, Prince Dube na never Tigere wapo katika kikosi chao kinachoshiriki fainali hizo wakati kwa Malawi yupo winga Peter Banda wa Simba.

Lakini kana kwamba haitoshi, ndani ya timu ya Zimbabwe, yupo kocha wa viungo, Nyasha Chandarura ambaye pia anaitumikia Azam FC.

Ushindi ni matokeo yanayohitajika kwa kila timu ili kuweka hai matumaini ya kutinga hatua ya 16 bora vinginevyo ile itakayopoteza inaweza kujikuta ikionyeshwa mlango wa kutokea kutegemeana na matokeo ya mchezo baina ya Guinea na Senegal ambao utachezwa leo pia.

Ikumbukwe Malawi na Zimbabwe ni watani wa jadi katika mashindano hayo kwani zote zinatokea katika kanda inayosimamiwa na Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Kusini mwa Afrika (Cosafa).

Kocha wa Zimbabe, Norman Mapeza alisema hawana kingine wanachokihitaji dhidi ya Malawi leo zaidi ya ushindi.

"Nina furaha wachezaji wangu wameamua kusahau kilichotokea dhidi ya Senegal. Sitofanya mabadiliko kwenye kikosi changu na kikubwa nimewasisitiza wachezaji kuendeleza ubora wao na kutumia vyema nafasi," alisema Mapenza.

Kocha msaidizi wa Malawi, Meck Mwase alisema kuwa wana matumaini ya kufanya vyema dhidi ya Zimbabwe leo.

"Tulikuwa na kiwango kizuri lakini tukakosa bahati dhidi ya Guinea. Tumejifunza kutokana na makosa yetu na tutakuja tofauti dhidi ya Zimbabwe. Tutakuwa na urejeo wa wachezaji ambao walikosa mechi ya kwanza. Zimbabwe ni timu nzuri kimbinu lakini nimewaambia wachezaji kuwa hii ni mechi ya lazima kwetu kushinda," alisema Mwase.

Timu hizo zipo katika kundi B linaloongozwa na Guinea na Senegal ambazo kila moja ina pointi tatu ikiwa imefunga bao moja mtawalia.

Reactions

Post a Comment

0 Comments