Ticker

6/recent/ticker-posts

DSTV BANNER

KUHUSU PABLO KUFUKUZWA ...MECKY MEXIME AWALIPUA MABOSI SIMBA...ADAI WAMEKURUPUKA KABLA YA KUFIKIRI...


Wadau wa soka nchini wamehimiza viongozi wa klabu mbalimbali waache tabia ya kujificha kwenye vivuli vya makocha na kuwabebesha mizigo ya timu zao za kufanya vibaya kumbe kuna tatizo ndani mwao.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti Jijini Dar es Salaam jana baadhi ya wadau wamesema hawapingani na suala la makocha kutimuliwa lakini wengi wanabebeshwa lawama wasizostahili wakati pengine kuna mambo hawajatimiziwa.

Kauli za wadau hao zinakuja ikiwa ni siku mbili zimepita tangu wekundu wa Msimbazi, Simba kutangaza kuachana na Kocha wake, Franco Pablo baada ya kushindwa kufanya vizuri kwenye ligi na michuano ya kimataifa.

Miongoni mwa wadau hao ni Kocha wa timu ya vijana Cambiasso, Mecky Maxime aliyesema kutimuliwa kwa Pablo na wengine kwenye timu za Ligi Kuu ni jambo la kawaida kwa makocha isipokuwa kuna baadhi ya viongozi wanaficha matatizo yao kwa makocha.

“Makocha wanafukuzwa, lakini viongozi wengi wanajificha kwenye vivuli vyao na kubebeshwa mzigo, je, kocha ametimiziwa mahitaji yake? Sioni Kama Kocha wa Simba alistahili kufukuzwa kipindi hiki,” alisema.

Maxime ambaye aliwahi kuzifundisha Mtibwa na Kagera Sugar alisema changamoto iliyopo mpira unaingiliwa na watu wasiokuwa na taaluma ndio maana fukuza fukuza ya makocha imekuwa kubwa.

Lakini haoni kama ina matokeo chanya akitolea mfano timu zote zilizofukuza makocha msimu huu hazijafanya vizuri mfano Azam FC, Namungo, Prisons, Biashara United na nyingine bado ziko vibaya.

Alisema anachokiona ni mihemko ya viongozi wengi wanakurupuka kabla ya kufikiri.

Kwa upande wake mchezaji wa zamani wa Majimaji ya Songea, Bebe Mapunda alisema kufukuzwa kwa makocha ni jambo la kawaida ila kile ilichofanya Simba ingempa muda kocha wao Pablo.

Alisema kwanini wasingemfukuza kipindi kile ambacho walikuwa wanashiriki michuano ya kimataifa? Kwasababu kuna mechi walianza kufanya vibaya wakiwa huko.

Naye mchezaji wa zamani wa Simba, Zamoyoni Mogella alisema kilichofanywa na Simba hakiwezi kupingwa isipokuwa kwa mtazamo wake, anaona kuna shida ndani ya uongozi.

Alisema haiwezekani Simba icheze michuano ya kimataifa kila mwaka inaishia robo fainali, ilipaswa kupiga hatua nyingine hivyo ni wazi klabu inatakiwa ijisafishe kuanzia kwenye uongozi, benchi la ufundi hadi wachezaji.

“Misimu mitatu hatuoni mabadiliko angalau kufika nusu fainali, sasa wakati umefika wa mabadiliko, kuna watu wamechoka kule waondolewe kuanzia kwenye uongozi,” alisema Mogella, nyota wa zamani wa Simba na Yanga.

Reactions

Post a Comment

0 Comments