Ticker

6/recent/ticker-posts

DSTV BANNER

KWA MARA YA KWANZA NTIBAZONKIZA AFUNGUKA CHANZO CHA KUTEMWA YANGA...ADAI HAKUPENDA..AITAJA SIMBA....


MARA baada ya Yanga kutangaza kuachana rasmi na Said Ntibazonkiza ‘Saido’, mashabiki na wadau wengi wa soka walishitushwa na taarifa hiyo wengine hawakuamini kabisa kilichotokea.

Hii inatokana na jinsi gani Saido alikuwa na mchango mkubwa ndani ya timu hii ndio iliwafanya watu wawe wagumu kuamini.

Mashabiki wa Yanga na wengine ambao sio wa timu hiyo hawakuamini kilichotokea lakini ilibidi wakubali tu matokeo.

Sasa kama ambavyo ilikuwa kwa upande wa mashabiki wa Yanga pia ilikuwa hivyo kwa mchezaji mwenyewe Saido ambaye pia hakuamini ambacho kilitokea.

Msimu huu Saido amefanikiwa kuichezea  Yanga mechi 17 huku akifunga mabao saba na ana asisti nne kwenye Ligi Kuu Bara.

ULIPOKEAJE TAARIFA ZA KUACHWA?

“Ni kawaida tu kwenye mpira, huwa inatokea sana mambo kama haya na unatakiwa uangalie ambacho kinafuata baada ya jambo kutokea na wala sitaki tena kuangalia nyuma.

WATU WANAJIULIZA SABABU ILIKUWA NI NINI?

“Barua ambayo wameiweka Yanga inaonyesha kila kitu ambacho kilitokea na mimi nimekubaliana na yote na ndio maana sikutaka kusema jambo lolote.

MKATABA MPYA ULIONEKANA KUCHELEWA SANA, KWA NINI?

“Ni kweli mkataba ulikuwa ni kikwazo kwa upande wangu na nakumbuka wakati imebaki miezi mitatu viongozi waliniambia kuwa tayari wameshaniandalia mkataba mpya na wangeniita kwa ajili ya mazungumzo lakini haikuwahi kutokea.

“Na wakati tunakwenda kucheza na Simba kule Mwanza nakumbuka mkataba wangu ulikuwa umebaki na siku kadhaa tu ili kuweza kukamilika.

“Mkataba wangu ulimalizika Mei 30, mwaka huu na kama utakumbuka ile mechi ilifanyika Mei 28 na hapo utaona kuwa zilikuwa zimebaki siku mbili tu ili mkataba umalizike.

“Na kama lisingetokea tukio la kuondoka kambini basi pengine ningecheza baadhi ya mechi za ligi mkataba ukiwa umemalizika.

LISINGETOKEA TUKIO LA KUONDOKA KAMBINI UNGESALIA YANGA?

“Sidhani na sina uhakika wa hili labda hii imekuwa ni sababu ya mimi kuondolewa ndani ya timu lakini viongozi waliniahidi kunipa mkataba mpya jambo ambalo hata mimi nakosa majibu

ULIKUWA NA MPANGO GANI NA YANGA?

“Mimi sikupenda kuondoka Yanga na wala sikuwa tayari kuondoka msimu huu na nilikuwa na malengo ya kwenda kuisaidia Yanga katika michezo ya kimataifa kwa msimu ujao.

“Na ndio maana nilikuwa nacheza vyema katika michezo yote ya ligi kuu nikiwa sina presha ya mkataba mpya nikiwa naamini kuwa nitaupata tu mkataba mpya mwishoni mwa msimu huu.

TUTARAJIE KUKUONA WAPI MSIMU UJAO?

“Kwa sasa napumzika kwanza kuhusu klabu ya msimu ujao na kwani nawaza kuisaidia kwanza timu yangu ya taifa kisha hayo mengine yatafahamika huko mbeleni.

TETESI ZINASEMA KUWA SIMBA WANAKUHITAJI VIPI KUHUSU HILO?

“Tetesi hazijawahi kukosekana katika mpira na kama wao wananihitaji ni wao, ambacho mimi nakifikiria kwa sasa ni kumalizana na mambo ya timu ya taifa kisha kuhusu klabu ya kwenda kuichezea msimu ujao itafahamika huko mbeleni.

“Maana sio Simba tu Wabongo wameshanihusisha na timu zaidi ya Simba, nimeshaambiwa kuwa nimesaini Singida na timu nyingine hivyo kwa sasa tetesi zitakuwa nyingi sana lakini mwisho wa siku mimi ndio mwenye majibu kamili na nitaweka wazi muda ukifika.

TUTARAJIE KUKUONA KUCHEZA BONGO AU NJE YA NCHI?

“Popote ambapo Mungu atanijalia basi ndipo nitakapocheza, kuna ofa nyingi za kwenda nje ya Tanzania ambazo nilizipata wakati bado nikiwa na mkataba na Yanga na zote bado zipo hai hivyo ikitokea sawa,” alisema Saido.

1,314: Dakika alizocheza Saido kwenye ligi kuu msimu huu akiwa na Yanga

Reactions

Post a Comment

0 Comments