Ticker

6/recent/ticker-posts

DSTV BANNER

SIKU CHACHE BAADA YA PABLO KUTIMULIWA...SIMBA WAANIKA IDADI YA MAKOCHA WALIOTUMA MAOMBI YA KAZI...


Klabu ya Simba imesema kuwa imepokea maombi kwa simu na barua pepe kutoka kwa mawakala na makocha mbalimbali duniani wakitaka kibarua cha kuifundisha timu hiyo kwa ajili ya msimu ujao, baada ya kumtimua kocha wao Pablo Franco.

Pamoja na hayo, klabu hiyo imesema imekuwa ikiingia makubaliano na baadhi ya wachezaji, lakini haijaanza rasmi usajili hadi hapo itakapitia ripoti ilioachwa na kocha aliyepita, lakini na mapendekezo ya kocha mpya atakayekuja.

Meneja Habari na Mawasiliano wa klabu hiyo, Ahmed Ally amesema jana tangu ilipoachana na kocha Pablo na kutangaza rasmi Mei 31, imekuwa ikipata maombi kutoka kwa makocha mbalimbali kurithi mikoba yake.

"Kuna wakati kila baada ya saa moja tunapata simu pamoja na barua pepe, lakini tangu kocha aondoke tumepata maombi mengi kutoka kwa mawakala ambao wamekuwa wakituambia wana makocha wazuri, pia makocha wenyewe kutoka pande mbalimbali za dunia wamekuwa wakitupa wasifu wao ili tu kuisaka kazi ya kocha aliyepita.

Kumiminika kwa maombi haya siyo kwamba kuna uhaba wa ajira la hasha, ila ni kwa ajili ya ukubwa na Simba, kila kocha mkubwa na mwenye viwango angependa kuja kuifundisha Simba, lakini hiyo haitufanyi sisi tuingie kwenye presha hizo, tutakaa na kuangalia nani atatufaa.

Hata sisi tunafuatilia mpira tunafahamu makocha wazuri, kwa hiyo atakayekidhi vigezo ndiyo atakayekuwa kocha wa Simba na tunawaahidi wanachama na mashabiki wa Simba tutawaletea kocha mwenye viwango vya dunia." Alisema.

Kuhusu usajili alisema harakati za kuingia makubaliano zimeanza, lakini hawajaanza usajili rasmi.

"Usajili hatujaanza rasmi, tumeelekeza jicho kusaka kocha, tukimpata kocha ndani ya wiki hizi mbili, ndiyo tutaanza mipango ya kukaa na kocha kutuambia anataka wachezaji wa aina gani na yeye aone wachezaji waliopo.

Mapendekezo ya kocha aliyepita na kocha mpya ndiyo yatatuelekeza na kutupa mwanga na taswira ni aina gani ya wachezaji ambao tunakwenda kuwasajili." Alisema Ahmed.

Reactions

Post a Comment

0 Comments