Home Habari za michezo BAADA YA KUFANIKISHA TAMASHA BAB KUBWA ….SIMBA KWA KUJIAMINI WAIBUKA NA KAULI...

BAADA YA KUFANIKISHA TAMASHA BAB KUBWA ….SIMBA KWA KUJIAMINI WAIBUKA NA KAULI HII YA KIBABE…YANGA MKIMBIEE….


TUMERUDI sasa. Ndivyo wanavyotamba mashabiki wa Simba baada ya msimu ulioisha kutowaendea vizuri na sasa wamefanya uamuzi mgumu kwa kuwatupia virago baadhi ya mastaa waliowaangusha na kushusha majembe mapya ambayo wanaamini yatawarudisha kwenye makali yao ya misimu minne iliyotangulia.

Msimu huu Simba imenasa mashine zaidi ya tano za maana na zenye uzoefu wa michuano mikubwa akiwamo beki wa kati kitasa Mburkina Faso Mohamed Ouattara kutoka Al Hilal ya Sudan, viungo washambuliaji Mghana Augustine Okrah, fundi Mzambia Moses Phiri na Wanigeria Victor Akpan na Nelson Okwa.

Simba imeongeza nguvu kwa kusajili wazawa wenye uzoefu na ligi, mshambuliaji Habib Kyombo aliyekuwa Mbeya Kwanza na kiraka Nassoro Kapama kutoka Kagera Sugar.

Wanamsimbazi hawajaishia hapo tu kwani wameshusha benchi la ufundi jipya kwa kumkabidhi timu kocha Mserbia Zoran Maki na Sbai Karim kuwa kocha wa viungo sambamba na kocha wa makipa Mohammed Rachid na kumbakiza Selemani Matola ambao wote wanaamini msimu huu utakuwa bora kwao.

MSIKIE ZORAN

Baada ya kukaa na timu kambini kwa siku kama 21 jijini Ismailia, Misri, Zoran alikiona kikosi chake na kuweka wazi Simba itakuwa kati ya timu tishio Afrika.

Anaeleza kufurahishwa na maufundi ya wachezaji wa timu yake ambayo anaamini kupitia mbinu zake timu itarejea kwenye heshima ya kutwaa makombe na kucheza soka la kuvutia katika michuano ya ndani na nje ya nchi.

“Timu ni nzuri, wachezaji wote wana vipaji vya hali ya juu na ina uwiano wa mchezaji zaidi ya mmoja kwa kila eneo jambo ambalo kila kocha analihitaji ili kuwa na machaguo mengi,” anasema Zoran mwenye uzoefu na soka la Afrika na kuongeza;

“Malengo ni kufika mbali kimataifa na kushinda mataji ya ndani, kila mechi kwetu itakuwa fainali na naamini kwa ushirikiano wa kila mmoja wetu tutairudisha Simba kwenye makali yake.”

Zoran akiwa na Simba ana kibarua cha kurejesha makombe ya ligi na lile la Shirikisho (ASFC) pamoja na Ngao ya Jamii yaliyoenda kwa watani wao Yanga msimu uliopita na kubwa kuliko msimu huu ni mkakati wa kufika nusu fainali ya Ligi ya Mabigwa Afrika.

MASTAA WATULIZA PRESHA

Baada ya kuambiwa ukubwa wa Simba hususani kwenye soka la Afrika, mastaa wapya wa timu hiyo wametuliza presha na kuahidi kufanya makubwa zaidi na kurejesha furaha iliyokosekana msimu uliopita.

SOMA NA HII  KARIAKOO DABI YAWAPA SAPRAIZI HII GAMONDI NA BENCHIKHA...WABAKI MIDOMO WAZI

Mshambuliaji Phiri aliyesajiliwa akitokea Zanaco ya kwao Zambia alikomaliza msimu na mabao 14, alieleza kuifahamu Simba tangu yupo huko na sasa amekuja Bongo kufanya kazi.

“Nimeifahamu Simba tangu nipo nyumbani, ni timu kubwa na imekuwa ikishiriki mara kwa mara michano ya Caf. Sambamba na hilo nina marafiki hapa mfano Clatous Chama na Rally Bwalya aliyeondoka hivyo ni kama nimekuja nyumbani,” anasema Phiri na kuongeza;

“Najua shauku ya mashabiki ni kutaka kupata matokeo bora kwenye kila mchezo na mimi nawaahidi kushirikiana na wenzangu kuhakikisha tunapambana hadi mwisho kuwapa furaha.”

Beki mpya Ouattara mwenye uzoefu na soka la Afrika ameeleza ameamua kujiunga Simba kutokana na ubora wake katika michuano ya Afrika huku akiamini ataongeza kitu msimu huu na kuipaisha juu zaidi nembo ya Mnyama.

“Simba ni timu kubwa, nimekuja hapa kufanya kazi ili kufikia malengo ya timu na yangu binafsi. Kila mmoja anajua ukubwa wa timu hii hivyo tupo hapa kupambana na kuhakikisha hatuwaangushi,” anasema Ouattara.

Nahodha John Bocco aliwataka mashabiki kutokuwa na wasi wasi kwani jeshi lao lipo tayari kuwapa furaha.

“Hatukuwa na msimu mzuri nyuma, ila sasa tumejipanga kurejea kwenye makali yetu na mashabiki wanahitaji kuwa na subra tutawafurahisha,” anasema Bocco.

VIONGOZI WAONGEA

Mtendaji Mkuu wa Simba, Barbara Gonzalez amefunguka kufanyia kazi upungufu uliojitokeza kwa msimu uliopita na sasa wamejipanga kuhakikisha wanarudisha heshima yao.

Anasema wameyabaini na kuyafanyia kazi maeneo yaliyowanyia ubingwa msimu uliopita na sasa wanaenda kuwafurahisha mashabiki wote wa Simba.

“Mpango wetu kwa msimu uliopita haukukamilika licha ya kwamba hatukufanya vibaya sana.

Msimu huu kila kitu kiko vizuri na tunawaahidi makubwa zaidi mashabiki wa Simba na hata wale wasio mashabiki wetu wataipenda tu,” alisema Barbara.

Mwenyekiti wa Simba, Murtaza Mangungu ameeleza msimu huu timu yake haitaki mazoea na inarudi kwenye ubabe wote wa miaka ya nyuma.

“Kwa usajili tulioufanya moja kwa moja unaona tumedhamiria kufanya makubwa zaidi, tuna mipango bora ndani na nje ya uwanja na tunaenda kurejea kwenye ubora wetu Simba ile hatari,” anasema Mangungu.