Home Habari za michezo KUELEKEA MECHI YA NGAO YA JAMII ….MANULA APEWA SIKU SABA KWA YANGA…KOCHA...

KUELEKEA MECHI YA NGAO YA JAMII ….MANULA APEWA SIKU SABA KWA YANGA…KOCHA AFUNGUKA ATAKACHOMFANYA..


KOCHA msaidizi na mtaalamu wa viungo Simba, Karim Sbai amesema kwa muda wa wiki mbili aliokuwa kwenye kikosi hicho amefanikiwa katika maeneo mengi tofauti na alivyokuwa akitegemea na kwamba wapo tayari kwa vita ikiwamo pambano lao la watani dhidi ya Yanga. Kocha huyo, licha ya kuwakosa nyota watano waliokuwa katika timu ya taifa, Taifa Stars, akiwamo kipa Aishi Manula, bado anaamini siku saba za kukutana nao jijini Dar es Salaam zitamtosha kuwapika kabla ya kuvaana na Yanga kwenye Ngao ya Jamii.

Sbai alisema anajua cha kufanya na wachezaji watano walioshindwa kuwepo katika kambi hapa Misri kutokana na kuwepo katika majukumu ya Taifa Stars huku mmoja, Sadio Kanoute akishindwa kusafiri kutokana na masuala ya hati ya kusafiria.

“Wachezaji wote hao nimewapa programu maalumu ya kufanya ya mazoezi yao binafsi na nikifika Tanzania kabla ya kujiunga na wenzao nitawaangalia wamefikia wapi ili kufahamu kama kuna cha kuongeza au kupunguza,” alisema Sbai na kuongeza;

“Baada ya hapo ndio nitawapa ruhusa ya kujiunga na wenzao katika siku chache za maandalizi ya Simba Day pamoja na ile wiki moja ya kujiandaa kucheza na Yanga.”

Pamoja na Manula, wachezaji wa Simba waliokuwa katika kikosi cha Stars ni Mohammed Hussein, Kibu Denis, Mzamiru Yassin na Kennedy Juma.

Sbai alifichua pia kuwa wakati anafanya uamuzi wa kuja kufanya kazi Simba hakuamini kama atakuja kukutana na wachezaji wenye viwango kama waliopo kikosini humo wakati huu.

Alisema alikuwa anasikia katika maeneo mbalimbali kuhusu Simba haswa katika Ligi ya Mabingwa Afrika ila hakuamini kama wanaweza kuwa na wachezaji bora, kumpata kocha mkubwa kama, Zoran Maki kuishi kwenye kambi nzuri kama waliyopo sasa pamoja na mambo mengine ya msingi.

“Baada ya kuanza kazi kuna wachezaji niliwakuta hawakuwa katika hali nzuri ya utimamu wa miili pengine sababu walitoka katika mapumziko ya msimu na hawakuwa na kocha wa viungo katika siku za hapo awali,” alisema Sbai na kuongeza;

SOMA NA HII  SAKATA LA HAJI MANARA NA BABBARA, SIMBA WATOA TAMKO

“Baada ya kufanya nao mazoezi kuna wachezaji ndani ya muda mfupi walianza kubadilika na kupokea kile ambacho nawapatia na miili yao kuwa sawa katika hali ya ushindani wa michezo mingi mfululizo.

“Si vyema kuwataja majina wale ambao wameimarika zaidi katika ushindani na wale ambao naendelea kupambana nao taratibu hadi kubwa vile ambavyo nahitaji kuona kutoka kwao na hilo halitawezekana kwani ndio jukumu langu.

“Kutokana na programu zetu za mazoezi nahitaji kutokuwa na wachezaji wenye majeraha, wanatakiwa wote kuwa tayari kuipigania timu kutokana na ratiba zangu za mazoezi, hilo linawezekana ili kuepuka changamoto ya msimu uliopita.” Katika hatua nyingine Sbai alisema mbali ya utaalamu huo wa viungo atakuwa akisaidiana na Selemani Matola kumpatia Zoran usaidizi wa kutosha kabla na baada ya mechi ili kuhakikisha wanafanya vizuri kwani hayo ni mafanikio ya wote.