Home Habari za michezo WAKATI YANGA WAKIMNGOJA KWA HAMU MANZOKI….BUMBULI ATUPIWA VIRAGO KIMYA KIMYA…MRITHI WAKE NI...

WAKATI YANGA WAKIMNGOJA KWA HAMU MANZOKI….BUMBULI ATUPIWA VIRAGO KIMYA KIMYA…MRITHI WAKE NI HUYU HAPA….


Huko Yanga hakuna kulala, ni mwendo wa bandika bandua tu. Wakati Rais Hersi Said akitaja safu ya uongozi atakayofanya nayo kazi, Kamati ya Tamasha la Wiki ya Mwananchi imetangaza mipango yake ya wiki nzima.

Kilele cha Wiki ya Mwananchi kinatarajiwa kufikia Jumamosio hii ya Agosti 6 kwa mabingwa hao wa Ligi Kuu Bara kucheza dhidi ya Mabingwa wa Ligi Kuu Uganda, Vipers kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Vipers ndiyo timu ambayo anaichezea straika Cesar Lobi Manzoki ambaye tayari amemwaga wino Simba, lakini dili lake halijakamilika kwani inadaiwa ana mkataba wa miezi miwili na timu yake.

Manzoki hajajiunga na Simba kutokana na waajiri wake kutaka Dola 200,000 (zaidi ya Sh400 milioni) ili kuvunja mkataba wake, jambo ambalo linaonekana kuwa gumu kwa Simba.

Juzi Agosti Mosi, Yanga iliweka mipango hiyo wazi katika hafla ya uzinduzi wa Wiki ya Mwananchi iliyoongozwa na Mjumbe wa Kamati ya Tamasha la Wiki ya Mwananchi, Taji Liundi ambaye pia ametajwa kuwa Mkurugenzi mpya wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano akichukuwa nafasi ya Hassan Bumbuli.

Liundi alitangaza kauli mbiu ya Wiki ya Mwananchini kuwa ni ‘Byuti Byuti’.

“Kauli mbiu hiyo inatokana na kile kitakachokuwa kinafanywa na wachezaji uwanjani, wataanza kuonyesha ufundi wao kuanzia Agosti 6, Yanga hatushindwi na jambo, msimu ulioisha kauli mbiu yetu ilikuwa ‘Yanga Tuna Watu’ na watu wakadhihirisha,” alisema

Alitaja ratiba itakavyokuwa baada ya kuanza na uzinduzi huo utakaoambatana na kutembelea vyombo vya habari, kuwa leo itakuwa ya kurudisha kwa jamii na aliweka wazi watatembelea Shule ya Sekondari Jangwani ya wasichana pamoja na kutoa mahitaji maalumu kwa wasichana.

“Tunawahimiza wananchi katika matawi ya Yanga waanze kutengeneza programu za kuisaidia jamii, lakini kwa kuwasaliana na makao makuu ili kuwapa msaada, Jumatano (kesho) ni siku muhimu kwa mdhamini mshirika, tutatembea kutoka makao makuu CRDB hadi Jangwani tukiwa tumevaa jezi zetu, itakuwa saa 11:00 jioni,” alisema na kuongeza;

“SportPesa ratiba yao itakuwa Alhamisi itakuwa ni uchangiaji wa damu, watashirikiana na Hospitali ya Muhimbili, hii ni muhimu kusaidia wananchi wenzetu, likiwezekana lifanyike hadi mikoani. Ijumaa tuna kocha nguli Pitso Mosimane na Jumamosi itawasili timu ya Vipers.”

SOMA NA HII  KISA KOMBE LA SHIRIKISHO KUHARIBIKA MIKONONI MWAO...YANGA WATOA TAMKO ...BUMBULI ADAI LINA SKRUU...

Makamu wa Rais wa Yanga, Arafat Haji ambaye pia ni mwenyekiti wa mpito wa Kamati ya Tamasha la Wiki ya Mwananchi alisisitiza kutakuwa na matukio tofauti tofauti ya kusisimua Jumamosi.

“Litakuwa tamasha la kuandika historia na wataona kauli mbiu yetu ya ‘Byuti Byuti’, mabingwa tukicheza na mabingwa wenzetu Vipers, mashabiki wataona ufundi wa mastaa ambao tumewasajili,” alisema na kuongeza;

“CRDB watakuwa wadhamini mwenza katika tamasha hilo na wapo tayari kuwekeza kwenye mpira na wanaanza kwa kufanikisha Wiki ya Mwananchi na tutakuwa na matukio tofauti ya kijamii tutakayoshirikiana nao.

“Wanayanga popote mlipo tunaomba mjitokeze kwa wingi wenu na muwe mfano wa kushiriki sensa ya mwaka huu, kwani ili serikali iwe na maendeleo lazima tuhesabiwe,” alisema na kuongeza.

SAFU YA UONGOZI

Yanga pia imetaja safu mpya ya uongozi itakayoongozwa na Rais Hersi Said, Makamu ni Arafat na nafasi aliyoondoka Senzo Mazingisa ya Mtendaji Mkuu anakaimu Simon Patrick ambaye pia atakuwa Mkurugenzi/Sheria wakati Mkurugenzi wa Fedha ni Haji Mfikirwa.

Mhasibu ni Justina Kubila, Mkurugenzi wa Mashindano ni Saad Kawemba akichukuwa nafasi ya Thabit Kandoro, Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano ni Liundi badala ya Hassan Bumbuli.

Kwa upande wa benchi la ufundi litakuwa chini ya kocha mkuu Nasreddine Nabi, msaidizi wake ni Cedric Kaze ambaye pia ameongezewa majukumu mengine atakuwa mkuu wa timu zote za vijana akichukua nafasi ya Mwinyi Zahera, kocha wa utimamu wa mwili ni Helmy Gueldich na kocha wa makipa ni Milton Nienov.

Mratibu wa timu atakuwa Hafidh Saleh akichukuwa nafasi ya Karigo Godson, Meneja wa timu ni Walter Harrison, madaktari ni Youssef Ammir Mohamed (Physio), Shecky Mngazija na mtunza vifaa ni Mohamed Omar.

MASTAA KIBAO

Nyota kibao wa muziki akiwamo Marioo, Madee, Msagasumu na Sir Jay ‘Ni Huyo Huyo’, watatumbuiza katika tamasha hilo J’mosi.