Ticker

6/recent/ticker-posts

WAKATI MABOSI SIMBA WAKIKAA KIKAO KUMJADILI ....MGUNDA KAONA ISIWE 'SOO' ...KAAMUA KUJIZUGISHA KWA NJIA HII...


LICHA ya uongozi wa Klabu ya Simba kusema Kaimu Kocha Mkuu, Juma Mgunda ni miongoni mwa watakaojadiliwa pale Bodi ya Wakurugenzi itakapokaa kuwajadili makocha waliotuma wasifu wao kuomba kazi ya kukinoa kikosi hicho, mwalimu huyo amesema akili yake ipo kwenye kuzitafuta pointi tatu muhimu dhidi ya Mbeya City na baadaye kwenda kuwawinda Primeiro de Agosto ya Angola.

Simba wanaendelea kutumia mchezo wa Mbeya City kwa kutafuta pointi muhimu kufikia malengo yao ya ligi na kujiimarisha zaidi kwa mchezo wa kwanza wa raundi ya Kwanza wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Primeiro de Agosto.

Kikosi cha Simba kitakuwa na  kibarua kigumu ugenini kuwakabili Mbeya City, mchezo utakaochezwa Septemba 28, mwaka huu kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya na baada ya hapo wataikaribisha Dodoma Jiji Oktoba 2 kabla ya kuifuata Primeiro de Agosto kwa mchezo utakaopigwa kati ya Oktoba 7 hadi 9, mwaka huu.

Mgunda alisema baada ya mapumziko mafupi wamerudi uwanjani kufanyia kazi mapungufu yao pamoja na maandalizi kuelekea michezo ijayo ikiwamo dhidi ya Mbeya City.

Alisema kabla ya kuanza kujiandaa na mechi ya kimataifa, anafikiria zaidi pointi tatu muhimu dhidi ya Mbeya City, ambao ana anaamini utakuwa wa ushindani mkubwa kwa sababu ya ugumu wa ligi.

"Mechi zote ni muhimu kwetu, tunafanya maandalizi ya mechi iliyopo karibu yetu, kabla ya kucheza mchezo wetu wa hatua ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Primeiro de Agosto, tunahitaji kupata matokeo mazuri katika michezo yote," alisema Mgunda.

Wakati huo huo, uongozi wa klabu hiyo umesema Mgunda ni miongoni mwa makocha watakaojadiliwa pale Bodi ya Wakurugenzi ya Simba itakapokaa kujadili makocha walioomba kukinoa kikosi hicho.

Akizungumza jana, Dar es Salaam, Meneja Habari na Mawasiliano wa klabu hiyo, Ahmed Ally, alisema hata hivyo mchakato huo kwa sasa hauna presha sana kama ilivyokuwa awali kutokana na timu kuwa kwenye mikono salama ya Mgunda.

 "Mchakato wa kusaka kocha mpya unaendelea na unakwenda vizuri, bado tunaendelea kupitia maombi ili tupate kocha sahihi, kwa sasa presha siyo kubwa ya kutafuta kocha kwa sababu timu iko kwenye mikono salama chini ya Mgunda, kuna utulivu, na hiyo inatupa fursa sisi kutafuta kocha sahihi kwa makini zaidi bila presha, hatuhitaji kufanya makosa tena, tunafanya upembuzi yakinifu ili kupata kocha anayetufaa," alisema Ahmed.

"Katika makocha ambao wametuma maombi yakianza kujadiliwa na yeye Mgunda atakuwa kwenye mjadala, pamoja na makocha wengine, baada ya hapo maamuzi sahihi yatafanyika, sifa anazo na uwezo anao ni miongoni mwa watu ambao bodi itamjadli," alisema.

Katika hatua nyingine alisema vikosi vya timu ya wanaume na wanawake vimeingia kambini tayari kwa majukumu yanayowakabili.

"Kikosi cha timu ya wanaume baada ya mechi dhidi ya Nyasa Big Bullets kilipata mapumziko, kinaingia kambini leo (jana) saa tisa kinatakiwa kuwa kambini kabla ya kuelekea mazoezini Mo Arena Bunju, tayari kuanza maandalizi ya mechi ya Ligi Kuu Septemba 28 dhidi ya Mbeya City pamoja na raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Primeiro de Agosto.

"Pia kikosi cha timu ya soka ya wanawake, Simba Queens nacho kiliingia kambini Jumatatu kujiandaa na fainali za Ligi ya Mabingwa Afrika na Ligi Kuu," alisema Ahmed.

Wakati timu ya wanaume ikitarajia kucheza mechi yake kati ya Oktoba 7 hadi 9 nchini Angola, Simba Queens inatarajia kucheza fainali hizo zitakazofanyika nchini Morocco kuanzia Oktoba 30, mwaka huu ikiwa imepangwa Kundi A, pamoja na timu za AS FAR ya Morocco, Green Buffaloes ya Zambia, na Determine Girls ya Liberia.

Reactions

Post a Comment

0 Comments